SAFARI ZA NJE YA NCHI ZAMPONZA BOSI TAKUKURU. - Rhevan Media

SAFARI ZA NJE YA NCHI ZAMPONZA BOSI TAKUKURU.

KASI ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu inaendelea kutikisa na safari hii imemkumba kigogo mmoja wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) kutoka Makao Makuu Dar es Salaam.

Mtumishi aliyekumbwa na panga hilo ni Doreen Kapwani, ambaye aliponzwa na safari aliyoifanya nje ya nchi bila kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu rasmi uliotangazwa na Ikulu Novemba 23.
Kapwani alikuwa Msemaji Mkuu wa Takukuru lakini ameondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kusimamishwa kazi kwa zaidi ya miezi miwili.
Nafasi yake imechukuliwa na Tunu Muleli ambaye kwa sasa ndiye Msemaji Mkuu wa Taasisi hiyo, kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka katika taasisi hiyo.
Alipozungumza na Nipashe hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alithibitishia kuwa Tunu ndiye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo kwa sasa.
“Tunaye Msemaji wa Takukuru anaitwa Tunu mtafuteni yeye ndiye atakuwa anawapa taarifa zote kuhusu Takukuru,” alisema Mlowola alipoombwa ufafanuzi kuhusu masuala ya taasisi hiyo.
Nipashe ilimtafuta Tunu ambaye ingawa alithibitisha kuwa yeye ndiye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, alikataa kuweka bayana alipo Doreen.
Desemba 15, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hosea na kuagiza kusimamishwa kazi kwa maofisa wengine wanne wa taasisi hiyo.
Maofisa hao ni wale waliosafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu ambao ni Kapwani, Mary Mosha, Ekwabi Mujungu na Rukia Nakitasi.
Alipoingia tu madarakani, Rais Magufuli alizuia safari za nje siku chache baada ya kuapishwa akisema watumishi wa umma watakaokuwa wakitaka kwenda huko watalazimika kuomba kibali kutoka Ikulu, ikiwa ni mkakati wake wa kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.
Kapwani na maofisa wenzake hao wa Takukuru waliomba Kibali cha kwenda kwenye mkutano nje ya nchi Desemba mwaka jana, lakini walipoona kibali hicho kinachelewa kutoka waliamua kuondoka.
Ikulu ilibaini kuwa maofisa hao walisafiri bila kibali na ndipo ilipoagiza wasimamishwe kazi ambapo hadi sasa Takukuru imesema hatua za kinidhamu kwa maofisa wengine waliosafiri na Kapwani ziko katika ngazi mbalimbali.
Hatua ya kuzuia safari za nje ya nchi ikiwa ni jitihada za kubana matumizi haiwagusi watumishi wa kawaida pekee kwani hata mawaziri na manaibu wao wamekuwa wakiziona safari hizo kaa la moto.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa asilimia 99 ya mawaziri na manaibu wao hawajawahi kuonja safari ya nje ya nchi tangu waapishwe mwishoni mwa mwaka jana na badala yake wamejipangia safari nyingi za ndani.
Hilo lilithibitika pia wakati wa ujio wa Rais Truong Tang Sang Vietnam ambapo Rais Magufuli alitoa kibali kwa mawaziri wawilui tu kwenda nchini humo kwa ajili ya kujifunza masuala ya Kilimo na Viwanda.
Mawaziri wawili waliopata kibali hicho ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ambao hawajasafiri hata hivyo.
Waziri pekee anayeonekana kuvuka kizuizi hicho cha safari za nje ya nchi ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Augustine Mahiga, ambaye mpaka sasa kumbukumbu zinaonyesha kuwa ameshasafiri nchi saba.
Waziri Mahiga ndiye atafaidi safari za nje katika awamu ya tano kutokana na asili ya kazi yake na ndiye atakuwa akiambatana na Rais Magufuli atakapoanza kusafiri nje ya nchi.
MASHARTI KWENDA NJE
Novemba 23 mwaka jana, Ikulu ilisambaza waraka unaoweka masharti ambayo mtumishi wa umma anayetaka kusafiri nje ya nchi anatakiwa kuyafuata.
Sharti la kwanza kwenye mwongozo huo ni kwa mtumishi kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Pili, kwa mujibu wa mwongozo huo, maombi hayo yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda kwa Katibu ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wake na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Tatu, Mtendaji Mkuu wa Shirika au Taasisi apime maombi husika kama yana tija ama umuhimu wa kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kabla ya kuwasilishwa Hazina.
Sharti la nne lina vipengele vitano ambavyo vinapaswa kuzingatiwa wakati wa kuwasilishwa kwa maombi ya safari na kipengele cha kwanza ni chanzo cha safari husika, faida yake, umuhimu wa safari hiyo kufanyika na isipofanyika itaathiri nini.
Kipengele cha nne kinaongelea gharama za safari, kikiweka masharti yanayomtaka mwombaji aainishe gharama ya tiketi ya ndege, posho za safari husika, mlipaji wa fedha za safari na uwezo wa taasisi.
Kipengele cha tano cha sharti la nne kinamtaka mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na umma kama imewahi kufanyika huko nyuma.
ATHARI SAFARI ZA NJE
Akizindua Bunge, Novemba 23 mwaka jana, Rais Magufuli alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 pekee bilioni 356.3 zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari za nje.
Alisema miongoni mwa fedha hizo, Sh. bilioni 183 zilitumika kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh. bilioni 68 kwa ajili ya mafunzo ya nje na posho za kujikumu ziligharimu Sh. bilioni 104.5.
Previous
Next Post »