BUNGE KUACHWA NJIA PANDA MKATABA WA LUGUMI. - Rhevan Media

BUNGE KUACHWA NJIA PANDA MKATABA WA LUGUMI.

  • Lakanusha kuudai wakati Katibu Mkuu Mambo ya Ndani, Mwenyekiti PAC wakikiri kudaiana mkataba huo...
KATIKA hali inayoonyesha kuwa suala la mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) sasa unaliogopesha Bunge,.....

Muhimili huo wa dola jana ulitoa taarifa inayopingana na maelezo ya mmoja wa wenyeviti wa kamati za chombo hicho cha kuisimamia serikali.
Akizungumza na Nipashe juzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema ofisi yake ingewasilisha mkataba huo kwa wakati kama ambavyo Bunge limeagiza.
Jenerali Rwegasira alikuwa akizungumzia amri ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Aprili 5, mwaka huu kutaka mkataba wa Polisi na Kampuni Lugumi wenye thamani ya Sh. bilioni 37 ambao unakabiliwa na hofu ya kujaa ufisadi uwasilishwe kwake kwa ajili ya kukagua makubaliano baina ya pande hizo mbili.
Lakini taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge ilisema taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha umma.
Badala yake, Bunge limedai katika taarifa hiyo kwamba,kamati ya PAC iliyokutana mwanzoni mwa mwezi huu ilibaini dosari katika utekelezaji wa mkataba huo hivyo kudai Katibu Mkuu huyo kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge.
Taarifa hiyo ya Bunge ilisema lengo lilikuwa PAC iweze kuchambua na kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua.
Akizugungumza na waandishi wa habari Jumanne iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilaly alisema kamati ilitaka mkataba huo ili kuwezesha wabunge kuangalia utekelezaji wake.
“Jana (Aprili 11) ilikuwa siku ya mwisho kwa jeshi kuwasilisha mkataba huo ofisi za Bunge, lakini mpaka leo (Aprili 12) muda huu ninapozungumza nanyi (saa 7:30 mchana) walikuwa hawajawasilisha," alisema Hilaly.
Mwenyekiti wa PAC huyo alikuwa akizungumza siku mbili baada ya jeshi hilo kudaiwa kukaidi agizo la kamati hiyo, ambayo ilitaka kufanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) katika hesabu za mwaka 2013/2014.
Kauli hiyo ya Jenerali Rwegasira ya juzi ilikuwa ikikinzana na kauli zake ambazo amekuwa akizitoa tangu PAC itake kupewa mkataba huo.
Moja ya kauli yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu huyo alisema licha ya kwamba wizara ndiyo inayosaini mikataba iliyo chini ya taasisi zake, kwenye kupeleka mkataba huo haihusiki kwa sababu PAC iliagiza polisi ndiyo iupeleke.
Kauli yake hiyo, ilitokana na ile ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Ernest Mangu, aliyetaka wizara iulizwe kwa madai kuwa wao ndio wanaohusika na mikataba mbalimbali ya taasisi zilizo chini yake.
“Sisi hatukuambiwa tupeleke mkataba huo kwenye kamati, kuna maelekezo maalumu tulipewa ambayo waandishi hamyajui,” alisema Jenerali Rwegasira alipozungumza na mwandishi wetu.
“Jeshi la Polisi lita-meet deadline (litatoa kwa wakati) mkataba huo.”
'Mkataba wa Lugumi' unaelezwa kuwa kaaa la moto kutokana na kuhusisha vigogo, baada ya kutajwa kwa jina la mtoto wa mmoja wa Marais wastaafu na IGP mmoja mstaafu kuwa washirika wa kibiashara wa mmoja wa wamiliki wawili wa kampuni hiyo, Said Lugumi.
Aprili 5,PAC ilikutana na viongozi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupitia mahesabu yao na kubaini kuwapo kwa mkataba huo tata ulioingiwa baina ya jeshi hilo na kampuni ya Lugumi wa ufungaji wa mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108 wenye thamani ya Sh. bilioni 37.
Lakini inasemekana ni vituo 14 tu ndivyo vina mashine hizo mpaka sasa, wakati kampuni hiyo ililipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote, hali iliyoilazimu PAC kuhitaji kupatiwa mkataba huo ili kuupitia.
Kati ya vituo 14 hivyo vilivyofungwa mashine hizo za kieleketoriniki ni vituo nane tu ndivyo vinafanya kazi, imedaiwa pia.
Baada ya kutupiana jukumu la kukabidhi mkataba huo kati ya IGP na Katibu Mkuu huyo, hatimaye PAC iliandikia barua na kulipa siku tatu hadi Aprili 15 (leo) Jeshi la Polisi liwe limewasilisha mkataba huo.
Ndipo ghafla ikaja taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge jana ikisema kuwa kinachotakiwa ni maelezo na si mkataba.
Taarifa hiyo ya Bunge inaonekana ni kama kutaka kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kujaribu kupotosha maagizo yaliyotolewa na kamati ya PAC ambayo inataka kuuona mkataba huo.
Previous
Next Post »