HATIMAE VIBARUA ZAIDI YA 888 KUSAINI MIKATABA. - Rhevan Media

HATIMAE VIBARUA ZAIDI YA 888 KUSAINI MIKATABA.

Zaidi ya wafanyakazi 888 wanaofanya kazi za ujenzi wa barabara ya Mangaka-Mtambaswala na Mangaka-Nakapanya wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara kwa kiwango cha lami, wamesaini mikataba baada ya agizo la Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi la kutaka wafanyakazi wa barabara kuwa na mikataba.

Wafanyakazi hao ambao wa makampuni ya Sichuan Road and Bdrige na Jiangxi Geo Engneering, walikuwa na mgogoro na makampuni hayo, ambao ulisababisha mgomo.
Ajira hizi zimekuja wiki chache tangu agizo la Waziri Profesa Makame Mbarawa alilolitoa mwezi uliopita la kuhakikisha wafanyakazi wa barabara wanakuwa na mikataba.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanroad Mkoani Mtwara, Aisha Amour alisema kuajiriwa kwa wafanyakazi hao 888 ambao awali walikuwa vibarua, ni utekelezaji wa agizo hilo la Mbarawa.
“Hapo nyuma kulikuwa na migogoro kwa miradi yote miwili, baada ya agizo la Waziri nilihakikisha natembelea makampuni haya ili kujiliridhisha endapo wafanyakazi wana mikataba," alisema Aisha.
Aisha alisema kampuni ya Sichuan inayojenga barabara ya Mangaka-Mtambaswala ina wafanyakazi 361, ambapo 242 tayari wana mikataba na wengine 90 wapo katika mchakato wa kupeleka vitambulisho vyao ili wapewe mkataba.
"Na tumekubaliana mpaka Jumatatu (kesho) mikataba hiyo itakuwa imesainiwa,” alisema Aisha.
Jiangxi Geo Engineering inayojenga barabara ya Mangaka-Nakapanya ina wafanyakazi 527, alisena na kati ya hao, 187 walikuwa wamepewa mikataba ya nyuma.
"Baada ya kuikagua watu wa 'labour' (Idara ya Kazi) wakagundua mikataba yao ilikuwa haijaboreshwa hivyo wakaagizwa kurudia upya hata hiyo mikataba ya nyuma, kwa hiyo nategemea Jumatatu nitakapokwenda watakuwa wamesainishwa."
Kwa mujibu wa Amour, ujenzi wa barabara ya Mangaka-Nakapanya yenye urefu wa kilomita 70.5 umefanyika kwa asilimia 50, na ulitarajiwa kukamilika Julai, mwaka huu.
Barabara ya Mangaka-Mtambaswala yenye urefu wa kilomita 65.5, imekamilika kwa asilimia 52, alisema. Ilitakiwa kuisha mwezi ujao, hata hivyo.
“Tulitegemea ujenzi wa barabara hizi zikamilike mwezi wa tano na saba, lakini kulingana na hali ya hewa, mvua zinaendelea kunyesha, wakandarasi wameleta maombi Tanroad la kuongezewa muda," alisema.
"Kwa kuwa mradi unasimamiwa na makao makuu wanaangalia bado, wanalifanyia kazi."
Previous
Next Post »