
Serikali imetoa muda wa siku 7 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari(TPA) mkoa wa Tanga, kurejesha mita ya kupimia mafuta(Flow Meters). Hatua hiyo ya Serikali inafuatia uamuzi wa TPA kuacha ufungaji wa mita hizo uliofanywa zaidi ya miaka mitano iliyopita ambapo kwa kipindi chote hicho Serikali ilikuwa ikiingia hasara na kupoteza mapato. Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi, Edwin Ngonyani wakati akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku moja iliyolenga kuangalia mwenendo wa utendaji wa Bandari ya Tanga. Katika ziara hiyo, pia Naibu Waziri alifanya ukaguzi wa Flow meters pamoja na matishari matatu ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne bila kufanya kazi bandarini hapo. Mhandisi Ngonyani alisema serikali imesikia kwamba kufungwa kwa mita za kupimia mafuta(Flow Meters)kwenye bandari za hapa nchini kumetokana na ushiriki wa baadhi ya wafanyakazi wa TPA waliokuwa wamelenga kunufaika kupitia wafanyabiashara wakubwa ambao kimsingi mita hizo zilikuwa zikiwabana katika ulipaji wa kodi. Pia imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hao wanajihusisha kufanya uchochezi kwa wananchi ambao walitakiwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mwambani, ambao licha ya kulipwa fidia lakini wameendelea kugoma kuachia ardhi hiyo. “Uamuzi wa kuondoa Flow meters ulikuwa ni wa kipuuzi kabisa na tumesikia uchochezi huu pia ulihusisha baadhi ya wafanyakazi," alisema Ngonyani. "Inasikitisha sana kwani nia yao ilikuwa ni kuwanufaisha wafanyabiashara."
Sign up here with your email