Chama cha Wananchi (CUF), kimedai kuwa Rais John Magufuli ameanza kuigeuka kauli yake juu ya amani na utulivu wa kisiasa visiwani Zanzibar baada ya kudai hataingilia mgogoro uliopo kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema hayo visiwani Zanzibar jana wakati akitoa tamko la CUF kuhusiana na kauli aliyoitoa Rais Magufuli mbele ya wazeee wa jijini Dar es Salaam juzi.Katika mkutano huo na wazee, Rais Magufuli alisema kamwe hataingilia mgogoro wa uchaguzi Zanzibar na badala yake anaiachia Tume ya Uchaguzi visiwani (ZEC) kuamua suala hilo kwa kuwa iko huru kama zilivyo tume zingine za aina hiyo duniani kote.Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Mazrui alisema Rais Magufuli amewashangaza CUF kwa kuwa kauli yake imeanza kupingana na kile alichokieleza Novemba 20, 2015, kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge 11 mjini Dodoma.“Rais Magufuli amejikanyaga na kujikanganya kwa kauli yake kwani wakati akizindua Bunge, alisema atalishughulikia tatizo la Zanzibar, lakini sasa anasema hawezi kuingilia mambo ya Zanzibar,” alisema Mazrui.