Waziri, George Mkuchika amefunguka na kuweka wazi mipango yake katika kutumikia nafasi yake na kusema yeye ataanza kuhakikisha watumishi wa Umma wanatumia muda wao kufanya kazi na hataki kusikia watumishi wameondoka makazini kwenda kunywa chai.
Waziri Mkuchika ambaye leo Oktoba 9, 2017 ameapishwa na Rais Magufuli kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa katika kipindi chake atahakikisha wafanyakazi wanalipwa mshahara kulingana na kazi zao kweli, na wanatumia muda wa kazi kufanya kazi za serikali.
“Kwanza katika kipindi changu nikiwa Waziri kwa watumishi wa Umma, nataka wananchi wanapofika maofisini wawakute maofisini, mara nyingi wengi wanaripoti ofisini baada ya muda wanaondoka wanasema wanaenda kunywa chai, yaani wananchi wanatoka vijijini wanamsuburi mtumishi aje eti ameenda kunywa chai jambo hili kuanzia leo nitasimamia kuhakikisha watumishi wa umma wanashinda kazini kwao ili kila mtumishi wa Umma alipwe mshahara kwa kufanya kazi muda wote” amesema Mkuchika.
Aidha Mkuchika amesema kuwa kwa sasa watumishi wengi wa Umma wanalipwa mshahara kamili kwa kufanya kazi robo za serikali jambo ambalo yeye atakwenda kulisimamia na kuhakikisha kuwa watumishi hao wanafanya kazi kamili ili walipwe kulingana na kazi zao kamili.
Mbali na hilo Mkuchika amedai kuwa atakwenda kuongea na Waziri wa Elimu ili ikiwezekana somo la Rushwa lianze kufundishwa kuanzia shule ya awali nchini mpaka vyuo vikuu na kusema watu wamekuwa wakichukua na kutoa rushwa kwa kuwa hawana elimu ya kutosha juu ya athari ya rushwa.
Sign up here with your email