ALICHOSEMA NDUGAI BAADA YA KASHILILA KUTUMBULIWA - Rhevan Media

ALICHOSEMA NDUGAI BAADA YA KASHILILA KUTUMBULIWA

Spika wa Bunge, Job Ndugai amemshukuru aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwa utumishi uliotukuka.

Ametoa shukrani hizo leo Jumatatu Ikulu jijini hapa baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha mawaziri, manaibu na Katibu wa Bunge mpya, Stephen Kagaigai.

Spika Ndugai pia amewakaribisha mawaziri, manaibu na katibu huyo bungeni mjini Dodoma.

“Ninyi mnatokana miongoni mwetu katika nyumba ile ya wabunge. Rais ameona awape nyadhifa hizi, kubwa na la kipekee nimkaribishe Katibu wa Bunge mpya Kagaigai na kipekee nimshukuru Dk Kashililah, asante sana kwa utumishi uliotukuka hatutakusahau,” amesema.

Amesema timu ya Baraza la Mawaziri ana imani nayo kwamba itafanya kazi vyema. Baada ya kuapishwa leo, watakutana katika kikao cha Baraza la Mawaziri.

“Mje Dodoma mmejiandaa, hii miaka miwili ya mwanzo walikuwa wanajifunza funza, sasa tukienda Dodoma itakuwa ni kazi tu,” amesema Spika Ndugai.

Wakati huohuo, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma amesema kile walichokitamka katika kiapo cha uadilifu wanapaswa kukizingatia kwa kufuata utaratibu wa kisheria na Katiba ili kuepusha migongano.
Previous
Next Post »