MTATIRO APEWA UJUMBE MZITO NA TUNDU LISSU AUFIKISHE KWA WATANZANIA - Rhevan Media

MTATIRO APEWA UJUMBE MZITO NA TUNDU LISSU AUFIKISHE KWA WATANZANIA

Mwenyekiti Kamati ya Uongozi katika Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, amesema kuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Mhe. Tundu Lissu, atarejea kwa nguvu zote na kwa kishindo kizito.
 
Mtatiro amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook kwa kuandika machache baada ya kumtembelea Mhe. Lissu hospitali Jijini Nairobi anapoendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika Septemba 7, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Area D, Mkoani Dodoma.
 
Mtatiro ameandika yafuatayo;
 
“SALAMU KUTOKA NAIROBI.
 
Mtatiro. J
Hapa jijini Nairobi leo nimepata fursa ya kumtembelea na kuzungumza kwa kirefu na ndugu yetu Tundulissu. Kama kuna mtanzania imara, asiyeogopa na mwenye maono makubwa ni Lissu. Lissu hana wasiwasi and he will strike hard very soon!
 
Risasi zote zilizopenya kwenye mwili wa Lissu zimemtengenezea uimara maradufu, mara sabini, mara mia moja. Waliodhani kuwa kumuua Lissu ndiyo kuua harakati za Watanzania kudai taifa la haki na linalofuata misingi ya sheria na katiba bora, wanajidanganya.
 
Lissu ameniambia “Mtatiro nenda kawaambie kuwa nitarudi nikiwa mzima na tutaendelea na mapambano maradufu zaidi, faraja muhimu nayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi sasa ni kuendeleza mapambano ya kudai haki na kupambana na udikteta, tusikubali nchi yetu iharibiwe na kikundi cha watu wanaoogopa kukosolewa”
 
Nimemwambia Lissu fikra zangu, kuwa “..siku nilipotaarifiwa kuwa umepigwa risasi nyingi ikiwa ni njia ya kukuua, nilitabasamu, nilijua mapambano ya kudai haki yamekolea, nilijua umekuwa imara mno maishani mwako na kwamba mateso utakayopitia yatakujenga na yatatujenga sisi zaidi!”
 
Mimi binafsi kama Mtatiro, kumuona Lissu kumenijenga zaidi, kumenifundisha kuwa ukipigwa risasi hata 100 kwa sababu u mkosoaji wa watawala yapo mambo mawili yatatokea, aidha utapona kama Lissu au utakufa kama ilivyowatokea wapigania haki wengi.
 
Uki-survive kama Lissu jambo moja litatokea, utaungana na wananchi wote kupigania haki kwa nguvu kubwa zaidi. Ukiuawa kwa risasi kama wapigania haki wengi jambo moja kubwa litatokea, kifo chako kitapandikiza mbegu kubwa ya ukombozi, kifo chako kitaliamsha taifa kupigania haki na kupambana na madikteta wajinga.
 
Kama wapuuzi waliomshambulia Lissu walidhani kuwa wanatutisha, kutuogofya na kuturudisha nyuma, wanajidanganya. Wanatuandaa kimwili na kiroho kulipigania taifa na kupambana kudai utawala wa haki, utawala wa sheria na katiba bora. Wanatuandaa kujitolea maisha yetu kwa ajili ya Taifa.
 
Nataka kuwaambia watanzania kuwa nchi yetu siyo Rwanda, siyo Burundi, siyo Congo wala siyo Uganda. Zipo njia zilitumika kuwazoesha Wanyarwanda, Warundi, Waganda na Wakongo udikteta. Kama yupo mtu anadhani anaweza kuipeleka Tanzania udiktetani anajidanganya. Tutalipigania taifa letu, utu wetu na uhuru wetu wa kuzaliwa bila kuogopa mikanda ya risasi.
 
Salamu kutoka Nairobi, he is going to strike soon and we will strike with him, harder and harder!
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
The Civic United Front (CUF),
08 Oktoba 2017 – Nairobi, Kenya.”

Previous
Next Post »