NYALANDU ALIVYOJITOA MUHANGA SAKATA LA TUNDU LISSU - Rhevan Media

NYALANDU ALIVYOJITOA MUHANGA SAKATA LA TUNDU LISSU

Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amesema kitendo cha Tundu Lissu kusalimika kifo kwenye tukio la kupigwa risasi ni Mungu tu ndiye aliandika, lakini kinamuumiza zaidi huku akilaumu ameikosea nini nchi mpaka kufanyiwa hivyo.

Kupigwa risasi kwa Lissu, ambaye alikuwa Dodoma kutekeleza majukumu yake ya kibunge, kuliwaibua wabunge walioliomba Bunge kuunda timu ya kwenda jijini Nairobi kumjulia hali mwenzao, lakini kiti cha spika kilikataa hoja hiyo kwa maelezo kuwa tayari baadhi yao walishaenda kuwawakilisha.

Wabunge ambao wakati huo walikuwa Nairobi ni Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai, na Mchjungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini wa chama hicho.

Wakati wabunge wakilalamika kukosa ruhusa ya Bunge, kulikuwa na malumbano kuhusu ushiriki duni wa Serikali na Bunge katika kumuuguza Lissu aliyepigwa risasi katika kipindi ambacho alishatoa malalamiko kuwa kulikuwa na watu asiowafahamu waliokuwa wanamfuatilia.

Lakini, Nyalandu alijitokeza na kwenda Nairobi kumuona Lissu, akiandika katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kuhusu safari hiyo na maendeeleo ya ziara yake, huku akituma picha zinazomuonyesha akiwa hospitalini.

Mbali na kumjulia hali na kuhimiza wananchi wamuombee, harakati za Nyalandu zimekuwa zikiambatana na ujumbe unaonekana kuwa na utata, ambao umemfanya atafsiriwe tofauti, akihimiza wananchi upendo, amani, kuvumiliana na haki kushinda dhuluma.

Pia, Nyalandu, ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2000, amelielezea tukio la kushambuliwa kwa Lissu kuwa ni kurudi nyuma kidemokrasia huku akiwaita waliomshambulia kuwa ni waonevu na kutaka Serikali ifanye jitihada kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki.

“Sote tuungane katika kufanya maombi maalumu kwa ajili ya #TunduLissu, na kwa wale walio karibu na mji wa Mbeya, naomba muungane nami katika Kanisa la Ebenezer,” ameandika Nyalandu katika ukurasa wake wa Instagram.

Katika video aliyotuma kwenye ukurasa huo, Nyalandu anasema:“Nimekuja Mbeya kulikumbusha Taifa kuwa kupigwa kwa mmoja wetu ni kupigwa kwetu sote, kuumizwa kwake ni kuumizwa kwetu sote, na kudhulumiwa kwake huyo mmoja ni dhuluma dhidi ya kila Mtanzania.

“Tundu Lissu amepona kwa kuwa imeandikwa (katiba Biblia) ‘hatasinzia yeye akulindaye’, na kwetu kama Taifa, tukasimama naye wakati huu wa kujaribiwa kwake. Naamini ndani ya moyo wake akiwa katika maumivu lukuki aliyonayo, #TunduLissu atakuwa anajiuliza nimekukosea nini Taifa.”

Wakati katika baadhi ya maeneo, watu walizuiwa kukusanyika kufanya maombi kwa ajili ya mwanasiasa huyo, Nyalandu anahimiza katika ujumbe wake kuwa Lissu aombewe “kimya, na tumwombee kwa sauti, tuombe mahali pa sirini, na tuombe hadharani”, akisema kuwa wameagizwa “kulia na wanaolia, kwenda kuwaona wagonjwa na waliofungwa, na tuwatangazie kufunguliwa kwao”.

“Naaam, hii ndiyo siasa sahihi ya utu kabla ya itikadi, upendo kabla ya visasi; heshima kabla ya husuda,” anasema Nyalandu.

“Watanzania wote tusimame, miguu yetu ikatiwe utayari, roho ya mapenzi na ujasiri ikatamalaki na kuondoa roho ya hofu na ganzi (spirit of indifference), tukaipandishe tena bendera yetu pale kileleni Kilimanjaro.

“Yamkini kwamba haki iishinde dhuluma; umoja wetu, ushinde roho ya matengano; na sauti za walioteswa na kuonewa zisikike na kuleta tena tumaini jipya la amani, haki, upendo, na mshikamano.”

Advertisement
==
Previous
Next Post »