Dar es salaam. Katika kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi, wanawake wenye ulemavu wameziomba taasisi za fedha kuwaamini na kupunguza riba kwenye mikopo wanayotoa ili waweze kukopa.
Ombi hilo linatokana na kundi hilo kutokuwa karibu na taasisi za fedha ambazo huwanyima mikopo wakidhaniwa kuwa hawana uwezo wa kuzirejesha licha ya kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Wakizungumza katika tamasha la jinsia leo Septemba 6 katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), wanawake hao wamesema wamesahaulika, hivyo kuendelea kuwa masikini.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wenye ulemavu kupitia shirikisho la wenye ulemavu nchini, Doris Kulanga amesema hakuna namna nyingine ya kuwasaidia wanawake zaidi ya kuwapatia mikopo yenye riba nafuu.
"Bahati mbaya tumeumbwa hivi tulivyo, tunanyanyapaliwa na kuachwa nyuma kwa sababu tunaonekana hatuwezi chochote. Mtuamini, tupeni mikopo rahisi tutairejesha," amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa shirika la Sightsavers, Angel Michael amesema ili kumuinua mwanamke mwenye ulemavu kiuchumi ni lazima sera za kiuchumi zimtaje.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Being'i Issa amesema kinachoweza kuwainua wanawake ni kujiunga kwenye vikundi vya kiuchumi ili iwe rahisi kukopeshwa.
Sign up here with your email

