MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amesema Bunge chini ya uongozi wa Spika Job Ndugai limekataa kugharamia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyepigwa risasi zaidi ya 38 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma,
Wakati Bunge likikataa kugharamia matibabu Kubenea amesema Spika Ndugai yeye aligharamiwa matibabu yake nje ya nchi kwa kipindi kirefu pamoja na aliyekuwa Spika mstaafu marehemu Samuel Sitta.
Amesema Bunge liliweka masharti kwamba ili Lissu agharamiwe matibabu yake ni lazima akatibiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na siyo nje ya nchi.
Mwanasiasa huyo amesema kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo Lissu asingeweza kufika Dar es Salaam kwa ndege ambayo ingetumia zaidi ya saa moja.
Hata hivyo, Kubenea amesema licha ya Muhimbili kuwa na watalaam wa kutosha, lakini hakuna vifaa ambavyo vingeweza kutumika kumtibu Lissu kutokana na hali aliyokuwa nayo siku hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kubenea leo amesema kesho atafika mjini Dodoma kwa ajili ya kuitikia wito wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo imeagizwa na Ndugai kumuita.
Ndugai ameagiza Kubenea afike mbele ya kamati hiyo kwa madai ya kujibu tuhuma za kumuita Spika muongo.
Amesema Lissu alipigwa risasi zaidi ya 38, wakati Ndugai anasema alipigwa mbili jambo ambalo limesababisha kumuita Ndugai kwenda mbele ya kamati ya Bunge.
Ameongeza kuwa suala siyo kubishania alipigwa risasi ngapi bali ni kilicho mbele ni kutaka Ndugai aseme nani kampiga Lissu risasi na kuhakikisha usalama wa wabunge.
Kubenea amemtaka Ndugai kuacha kuhangaika na vitu vidogo badala yake ajikite kujua ni nani aliyemdhuru Lissu na siyo vinginevyo.
”Lissu anaumwa sana, Lissu yupo mahututi, Lissu kaumia na madaktari wanaomtibu wanasema tofauti na anavyosema Ndugai kwamba alipigwa risasi mbili,” amesema.
Kwa upande mwingine, Kubenea amesema kinachosumbua siyo yeye kutaja idadi ya 38 bali, kalamu anayoitumia ili kukosoa utendaji wa Bunge chini ya Ndugai.
Kubene ambaye ni mwandishi wa habari, amekuwa mstari wa mbele kukosoa utendaji wa Spika kwa namna anavyoliendesha Bunge.
Amesema yeye hajasema Ndugai ni muongo bali alichotamka ndicho kimekuwa tofauti kwa hiyo haimaanishi kwamba amemuita muongo.
Akizungumzia kanuni za Bunge, Kubenea amesema Mbunge yoyote hakatazwi kuitoa taarifa yoyote anapokuwa nje ya chombo hicho na kwamba alichofanya yeye siyo kosa.
Ametolea mfano mjadala wa Richmond kulikuwa na watu mbalimbali waliokuwa wakiuzungumzia nje ya Bunge na hapakuwa na tatizo lolote.
Sign up here with your email