Dar es Salaam. Kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) leo imeziwashia taa ya kijani timu za Yanga na Singida United kuwatumia wachezaji Deus Kaseke na Obrey Chirwa waliosimamishwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu msimu iliopita.
Wachezaji hao wawili sambamba na Saimon Msuva anayecheza soka la kulipwa Morocco, walituhumiwa kumfanyia fujo mwamuzi kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu walipokuwa wanaichezea Yanga dhidi ya Mbao FC jijini Mwanza.
Makamu mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya TFF, wakili Peter Hela alisema kamati yake imekosa ushahidi wa kuwatia hatiani Chirwa ambaye bado yupo Yanga na Kaseke aliyesajiliwa na Singida United.
"Ukizingatia wachezaji hao tayari walishakosa mchezo mmoja wa ligi, kamati imeamua kuwaachia huru na kuishauri TFF izipe uhuru kamati zake katika kutekeleza majukumu," alisema Wakili Hela.
Kuhusu Msuva, wakili Hela alisema kamati imeamua kumuandikia barua ya karipio kutokana na kutocheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.
Sign up here with your email
