WAZIRI WA MICHEZO DKT.MWAKYEMBE AMPONGEZA MWENYEKITI WA BMT,DIONIS MALINZI KWA HATUA YA BARAZA KUZUIA VIONGOZI KUWA NA KOFIA MBILI KWENYE MCHEZO MMOJA - Rhevan Media

WAZIRI WA MICHEZO DKT.MWAKYEMBE AMPONGEZA MWENYEKITI WA BMT,DIONIS MALINZI KWA HATUA YA BARAZA KUZUIA VIONGOZI KUWA NA KOFIA MBILI KWENYE MCHEZO MMOJA

dioniznscchaneta
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe amempongeza Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dionis Malinzi kwa hatua kadhaa ambazo baraza lake limeanza kuchukua katika kusimamia michezo nchini, likiwemo zuio kwa viongozi kuwa na kofia mbili kwenye mchezo mmoja.
Katika salamu alizomtumia kiongozi huyo wa BMT jana jioni, Dk. Mwakyembe amesema hatua hizo zimeonesha uhai, uhalali na hitaji la uwepo wa BMT kwa maendeleo ya michezo nchini.
Dk. Mwakyembe amesema Wizara haitarajii tena kuona kiongozi katika mchezo wowote ule nchini kuwa na kofia mbili kinyume na sheria na kanuni zilizopo, huku BMT ikiangalia pembeni na kuinyamazia hali hiyo.
Waziri Mwakyembe vilevile amesema Wizara haitarajii kuona chombo chochote cha michezo nchini kikikiuka Kanuni na Sheria za nchi bila kuchukuliwa hatua stahiki kwa kisingizio kuwa kinawajibika kwa vyombo vya kimataifa, kwani kisingizio hicho ni batili kikatiba na kisheria hivyo hakiwazuii BMT kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Aidha amewapa pole BMT kwa kuondokewa na mwanamichezo maarufu nchini Ally Mohammed, a.k.a. Ally Yanga, aliyefariki dunia jana (Jumanne) kwa ajali ya gari wilayani Mpwapwa.
“Tumepoteza kifaa muhimu katika kuhamasisha michezo nchini na nifikishieni salamu zangu za rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu na wanamichezo wote nchini”, Dk. Mwakyembe amesema na kuwatakia BMT mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao.
Imetolewa na:
Genofeva Matemu
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
21/06/2017
Previous
Next Post »