MASHUJAA NYUMA YA VITA ESCROW - Rhevan Media

MASHUJAA NYUMA YA VITA ESCROW


Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
HAWA ndio vinara wa kupinga malipo ya zaidi ya Sh bilioni 300 zilizolipwa kwa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Limited (IPTL) kwa kuhakikisha hoja hiyo inasimamiwa imara na Bunge ili kupinga malipo hayo ya fedha.
Viongozi hao waliosimama na kupinga malipo hayo ni aliyekuwa Mkurungezi wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, aliyekuwa Kamishna wa TRA, Rished Bade, Spika Mstaafu wa Bunge la 10, Anne Makinda na Spika wa sasa Job Ndugai ambao kila mmoja alitumia nafasi yake kuhakikisha suala hilo linafika bungeni na wahusika wanachukuliwa hatua

Kusimama kwao imara kumekuja siku chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kuwafikisha mahakamani vinara wawili wa sakata hilo kuwaburuza mahakamani, Mwenyekiti wa Mtendaji IPTL/Pan Africa Power (PAP), Harbinder Sethi Singh na mwenzake wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd,  James Rugemalira.
Vigogo hao hao walifikishwa   katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19, mwaka huu na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa udanganyifu na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60  (Sh bilioni 309.5).
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kupelekwa rumande hadi Julai 3 kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.
Inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, mwaka 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, watuhumiwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.
VINARA
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amewataja vinara waliofanikisha vita dhidi ya uchotwaji wa fedha hizo kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya ufuaji wa umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na IPTL kuhusu kiwango kinachopaswa kulipwa na baadaye suala hilo kupelekwa mahakamani.
Fedha hizo zilitakiwa zitolewe baada ya mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo, lakini zilitolewa na kulipwa kwa mmiliki mpya wa Kampuni ya PAP na kusababisha kuibuka kashfa hiyo.
Baadaye ilionekana fedha hizo zikiingia katika akaunti za mawaziri, majaji, watendaji waandamizi wa Serikali, wabunge na watumishi wengine wa umma.
Kutokana na wabunge wengi kusimamia kidete suala hilo, baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijiuzulu huku viongozi wengine wakiwamo mawaziri nao wakiachia nafasi zao.
Awali, kabla watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, aliwaeleza waandishi wa habari jinsi alivyochukua muda kuchunguza suala hilo hadi kuamua kulipeleka mahakamani.
Kutokana na hali hiyo Zitto, amelazimika kuandika waraka mzito baada ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani na kusema suala lao limeleta msisimko mkubwa kwa jamii.
“Navuta picha ya mahakamani, namwona pia James Rugemalira mmiliki wa hisa asilimia 30 za IPTL na aliyeuza hisa hizo kwa Sethi kwa malipo yaliyotokana na fedha zilizoporwa kutoka BoT.
“Kisaikolojia picha ile ina maana kubwa sana kwenye vita dhidi ya ufisadi nchini. Rais Magufuli amefanya jambo la kiukombozi (psychological liberation),” alisema Zitto.
 VINARA VITA YA ESCROW
Alisema ni wazi kwamba mtu kama David Kafulila (aliyekuwa Mbunge Kigoma Kusini), siku watuhumiwa hao walipofikishwa mahakamani alikuwa na furaha sana kuona matunda ya kazi yake kwa sababu alisimamia kidete sakata hilo.
Zitto ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema wajumbe wote waliokuwamo katika kamati hiyo mwaka 2013-2015 wanastahili pongezi kwani wangekubali kugawanywa wangepoteza ajenda.
“Mshikamano tulioonyesha ilikuwa silaha kubwa. Wapo mashujaa ambao siwezi kutaja majina yao (Unsung Heroes), hawa ni wengi mno, wengine ni watumishi wa Bunge. Sitaki kuwataja, lakini vijana wale na mama yule chini ya Katibu wa Bunge walipata majaribu makubwa sana. Walisimama kidete,” alisema.
Katika waraka huo, pia aliwataja aliyekuwa Mkurungezi wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na watumishi wengine wa ofisi hiyo kwa namna walivyoisaidia kamati kwa kiwango cha juu.
“Mpaka leo nikimuwaza Hoseah kwenye sakata hili kama nimevaa kofia ninaivua kwa heshima kubwa sana kwake,” alisema Zitto.
Wengine aliowapongeza ni Kamishna wa TRA, Rished Bade akisema ndiye aliyekata mzizi wa fitina kwa kuithibitishia Kamati ya PAC ushahidi nyeti kuhusu masuala ya kodi.
Alisema ushahidi huo muhimu wangeukosa, pengine wasingekuwa na taarifa hiyo.
Pia alisema Bunge lilifanya kazi yake kwa ufahari kwa kulisaidia taifa kwa kuleta maazimio yaliyolipa heshima na kwamba anajivunia kuhudumu kwenye Bunge hilo la kumi.
Aidha alimkumbuka pia Makamu Mwenyekiti wake, marehemu Deo Filkunjombe (aliyekuwa Mbunge wa Ludewa), akisema suala hilo la Escrow limemuonyesha kuwa watu wema hawafi.
“Jambo hili la Tegeta Escrow limenionyesha kuwa ‘watu wema hawafi, hata kama miili yao iko mchangani tayari (kaburini)’, na hili ndilo linalojidhihirisha kwa ndugu na rafiki yangu wa karibu mno, aliyekuwa makamu wangu wa uenyekiti wa PAC, Deo Fulikunjombe. Miaka miwili tangu afariki sasa, bado taifa linakumbushwa juu ya uzalendo wake.
“Sijui Deo angekuwa hai angekuwa katika hali gani. Ninamlilia ndugu yangu. Kitu kimoja ambacho watu wengi hawajui ni kwamba muda wote wa kuandaa taarifa maalumu ya PAC kuhusu Tegeta Escrow, yeye ndiye aliandaa ulinzi wangu kuhakikisha sidhuriwi.
“Alimwambia dada yangu aje Dodoma kuhakikisha ninakula kile tu kilichopikwa na dada yangu. Shujaa wa kazi hii ni yeye,” alisema Zitto.
Alisema funzo kubwa muhimu katika kadhia hiyo ni umuhimu wa uhuru wa kiutendaji wa taasisi mbalimbali nchini.
“Taasisi huru husaidia uwajibikaji mahali penye makosa, husaidia kufichua ufisadi na huleta uwazi. Yawezekana bila uhuru wa Takukuru, CAG, BoT, TRA, vyombo vya habari pamoja na Bunge, leo nisingekuwa nazungumza haya, ni muhimu sana tupiganie na kulinda uhuru huu wa taasisi,” alisema Zitto.
Akielezea namna walivyopambana awali, alisema alishauriana na Filikunjombe ili ukaguzi ufanywe na CAG kuhusu suala hilo.
“Baada ya siku mbili tukamwita Gavana wa BoT, Benno Ndulu mjini Dodoma. Baada ya kikao kifupi PAC ikaagiza rasmi ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow. Tukaagiza taarifa iletwe bungeni na si wizarani.
“Mkakati huu ulitusaidia mno mbeleni kwani juhudi za Serikali kuzuia ukaguzi ziligonga mwamba maana mchezo wa wizara tuliushtukia na kuuzuia. PAC ilitoa taarifa kwa umma juu ya ukaguzi husika,” alisema Zitto.
Alisema katika mapambano hayo ambayo yalikuwa na vikwazo vingi, Kafulila akajitokeza kubeba jukumu la kuweka shinikizo kwa Serikali.
Mbali na hilo, alisema naye aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, alitoa msaada mkubwa kwa kamati na baadaye akatukanwa kuwa hakuwa msomi na kwamba kidato cha sita alipata sifuri.
“Mtindo huu wa kuvunjia watu heshima pia ulitumika dhidi yangu, kwa kutengeneza kijitabu cha propaganda kilichogawanywa kwa ustadi na mafanikio makubwa kwa kila mbunge nyumbani kwake mjini Dodoma,” alisema.
Zitto alisema baada ya kuona jamii haielewi kuhusu ufisadi huo, aliamua kutafuta fedha ili Kafulila azunguke mikoani kuwaelimisha wananchi kwa kugawa kitabu alichokiandaa kuhusu sakata hilo.
Alisema wakati huo PAP na IPTL nao waliongeza nguvu, huku sauti dhidi ya ukwapuaji ule ikiwa ni ya Kafulila na PAC tu jambo ambalo liliwafanya wavunjike moyo kwa sababu viongozi wengine wa vyama vya upinzani walikuwa kimya.
“Tulikuwa tunajiuliza nini hasa kimetokea? Tulipata nguvu ya pamoja baada ya hoja kufikishwa kwenye kamati na kwa makusudi kabisa kuvujisha baadhi ya taarifa kwenye vyombo vya habari ili kupata uungwaji mkono wa wananchi.
“Watu wa PAP/IPTL pia walikuwa na mikakati yao ya vyombo vya habari. Kwanza walicheza na taarifa ya CAG na kuisambaza kwa nguvu kabla ya taarifa rasmi kutolewa. Hawakujua kuwa sisi PAC tulikuwa na taarifa ya kwanza kabisa ya CAG ambayo ilikuwa na ukweli wote kabla ya taarifa yao iliyochezewa.
“Ndiyo maana kulikuwa na mchanganyiko mkubwa kwa umma kuhusu fedha ni za umma au si za umma, kwani ilikuwa ni mkakati maalumu wa wakwapuaji wa fedha zile,” alisema Zitto.
Alisema ili kujenga umoja ndani ya Bunge, alimwomba Spika Makinda kumwongezea wajumbe wa kamati, ombi ambalo alilikubali kwa kuwaongezea Kangi Lugola, Suleiman Zedi na Dk. Hamis Kigwangala.
Alisema wakati wakiendelea na harakati hizo, wakwapuaji hao nao walijipanga kwa kuwagawia fedha kila mbunge anayechangia.
“Sisi tuliamua kuwachezea mchezo wa kupanga wachangiaji wetu wazuri siku ya mwisho na wao wakaja kuchangia siku ya pili ya uwasilishaji wa taarifa bungeni, Filikunjombe alifanya kazi hiyo ya mkakati,” alisema Zitto.
Alisema Spika Makinda na kabla yake Naibu wake, Job Ndugai walitoa ushirikiano mkubwa.
“Ndugai alituambia wakati wa kukabidhiwa ripoti, namnukuu ‘waelezeni Watanzania ukweli. Nipo nanyi’. Kweli alikuwa nasi na ili kutupunguza nguvu akapewa safari ya ghafla kwenda Paris.
“Lakini Spika Makinda alikuwa ameelewa jambo hili vizuri sana. Alitupa mwongozo kama mzazi, kutoka mwanzo mpaka mwisho. Naushukuru sana uongozi wa Bunge.
“Pia tulijua kuwa wabunge wa CCM wakiweka msimamo wa kupinga, taarifa yetu itakwama. Siasa za kibunge uamuliwa kwa msingi wa demokrasia ya ‘wengi wape’. Wabunge wa CCM ndio wengi bungeni, ukitaka jambo lako ni lazima ujenge ushawishi kwao,” alisema.
Kutokana na ugumu wa vita hiyo, Zitto alisema ilimlazimu azungumze na aliyekuwa Katibu NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akiwa kwenye ziara mikoa ya kusini na kumwambia amwombe Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa kusiwe na msimamo wa chama chao kwenye jambo hilo kwa kuwaacha wabunge wao wawe huru kuzungumza jambo ambalo lilikubaliwa na kiongozi huyo.
“Filikunjombe akazungumza na mzee Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti wa CCM) ambaye alikuwapo Dodoma kumwomba hivyo hivyo. Mzee Mangula alimwuliza ‘kwa nini maazimio umesoma wewe na si mwenyekiti wako? Sio mtego kuwa wewe ndio unyonge CCM wenzako?’. Bahati nzuri jambo tulilipanga vizuri kabla,” alisema Zitto.
Alisema wakati huo alikuwa kwenye ugomvi mkubwa na chama chake Chadema, hivyo ikabidi ajisogeze kwao ili taarifa isipate mkwamo.
“Hata kamati ya kuandika maazimio tukawaweka watu kama Tundu Lissu na Freeman Mbowe na upande wa CCM, Anna Kilango Malecela ambaye mwanzoni hakuwa upande wetu. Tulifanikiwa kujenga mwafaka wa kibunge,” alisema.
Pamoja na hali hiyo pia aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, alipinga hatua ya fedha hizo kuitwa ni mali ya IPTL na kuhoji inakuwaje kama fedha hizo zingekuwa mali ya mtu binafsi kwa nini ilikaguliwa katika vitabu vya BoT.
Profesa Mwandosya alimpa pole Zitto kutokana na makombora alitokuwa akirushiwa huku akimtaka kutokata tamaa na asimame imara kwani Taifa litakumbuka mchango wake siku moja.
Wakati akisema hayo Lissu, alisema watu waliopewa fedha hizo ni wezi na hawastahili kutetewa kwani baada ya kuona kuna hatari ya suala lao kugeuka waliamua kugawa fedha kwa baadhi ya wabunge na watendaji wa Serikali.
Mbali na hao pia aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla, alisema kuwa Profesa Muhongo, alikuwa muongo kwani imekuwa ni kawaida yake kutetea uongo mara kila wakati.
WALIOTETEA UCHOTWAJI FEDHA
Pamoja na Kamati ya PAC kuwasilisha ripoti yake juu ya suala hilo ambapo ilijiridhisha kuwa sehemu ya fedha hizo ni za Serikali, baadhi ya wabunge na mawaziri walipinga hatua hiyo na kusema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma bali ni mali za IPTL.
Mmoja wa mawaziri waliosimama bungeni kutetea suala hilo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alizungumza kwa kujiamini kuwa fedha hizo si mali ya umma.
 LUSINDE
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), akichangia ripoti hiyo ya PAC bungeni, alisema hata Zitto ambaye ni mwenyekiti wa kamati alipokea fedha kutoka kwa Sethi.
“Zitto ni rafiki yangu mkubwa na aliwahi kunisaidia nilipokuwa na tatizo, lakini katika hili lazima niseme kwamba ulipokea fedha kutoka kwa Sethi, atupe jibu isije kuwa tunakaa hapa kumbe walaji wako wengi. Kwa nini Tibaijuka anapopewa inakuwa fedha haramu, lakini kwa Zitto ni halali?
“Na Zitto anahusika, Kafulila naye anakuja hapa ohh eti taarifa ya siri imevuja tujadili, tujadili kwani ninyi Mungu?” alihoji Lusinde.
 MOHAMED CHOMBO
Mbunge wa Magomeni, Zanzibar, Mohamed Chombo (CCM) alisema: “Nimesikiliza ripoti ya PAC na Serikali, lakini jambo hili lipo wazi kwamba hizi fedha hazikuwa za umma, zilikuwa za IPTL zimelipwa na Tanesco.”
 RICHARD NDASA
Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema kumezuka mtindo wa kusingiziana na kwamba wabunge wa aina wamwogope Mungu.
“Tusiwavunje moyo wizara, wamefanya kazi kubwa, tushauri pale kwenye tatizo tuseme sasa fukuza huyu halafu nini kinafuata?
“Tukiwa na utaratibu wa kufukuzana itaendelea hivyo hivyo, tumwogope Mungu, lakini nafsi zetu zitatusuta kwa sababu ya matendo yetu. Hivi sasa kamezuka mtindo wa kusingizia mtu huyu kala, huyu kapewa mtu akipewa asimame hapa aseme amepewa, lakini tusiwasingizie,” alisema Ndassa.
 MARIAM KISANGI
Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), alisema upinzani baada ya kuona kwamba chama tawala kinapeta wakaamua kuwakoroga na Escrow.
“Tuangalie utendaji wa watu na ninawaambia hatoki Muhongo wala Maswi, CCM kitapita na hiyo ndiyo njama zenu upinzani kutukoroga. Mmekaa mkao na CCM inapeta, mkajisemea hawa tuwakoroge na nini ndio mkaja na Escrow mara EPA, nawaambia njama zenu hazisaidii.
“Zile fedha si za umma. Tanesco ina madeni mengi, inadaiwa Sh bilioni 700. Waziri ameeleza vizuri, kwa hiyo tusipotezeane muda hapa,” alisema mbunge huyo. 
SIMBACHAWENE
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, naye alitumia mbinu zote kutetea ufisadi huo na wakati mwingine alijenga hoja ili watuhumiwa waweze kupenya.
Previous
Next Post »