MWANASHERIA MKUU TBS AKAMATWA TENA BAADA YA KUACHIWA HURU - Rhevan Media

MWANASHERIA MKUU TBS AKAMATWA TENA BAADA YA KUACHIWA HURU


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia kesi Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54) aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kuishi na kufanya kazi nchini bila kibali.

Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alimfutia mashtaka Mwanasheria huyo wa TBS leo (Jumatano) baada ya Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Method Kagoma kuiomba mahakama imfutie makosa hayo chini ya kifungu cha 98 (a) cha sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Hata hivyo baada ya mshtakiwa huyo kuachiwa huru alikamatwa tena na yupo katika Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya mahojiano.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay akimsomea mashtaka mshtakiwa huyo, alidai kuwa Mei 19, 2017 huko Kinondoni katika ofisi ya uhamiaji, Bitaho akiwa raia wa Burundi alikutwa akiwa nchini bila ya kuwa na kibali.

Imedaiwa kuwa, Bitaho siku hiyo alikutwa akifanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila ya kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya kazi hapa nchini.

Kadhalika, inadaiwa kuwa, Julai 6 mwaka 2011 katika ofisi ya Uhamiaji ya Dar es Salaam iliyopo Wilaya ya Ilala, mshtakiwa huyo akiwa raia wa Burundi alitoa taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi wakati akijaza fomu ya kuomba hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).

Wakili Mlay ameongeza kuwa, kitendo hicho cha kutoa taarifa za uongo kilimuwezesha Bitaho kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye namba AB 474856 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshitakiwa aliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja alisaini bondi ya Sh 20 milioni.
Previous
Next Post »