KAMUSI YA KISWAHILI NDANI YA SIMU ZA KIGANJANI - Rhevan Media

KAMUSI YA KISWAHILI NDANI YA SIMU ZA KIGANJANI

Tokeo la picha la KAMUSI YA KISWAHILI NDANI YA SIMU


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtafiti wa Kamusi ya Kiswahili kwenye simu za mkononi Dk George Mrikalia akionyesha namna kamusi hiyo inavyofanya kazi wakati wa maonyesho ya wiki ya tafiti UDSM 

Upo msemo; ‘kila zama na kitabu chake’ Kwa hakika zama za kutembea na kamusi kwenye begi au mfuko zimeshapitwa na wakati.
Siku hizi sio kama zamani tena, zama za sasa zinazungumzia zaidi matumizi ya simu za mkononi.
Simu imekuwa njia rahisi zaidi ya kufikisha ujumbe na huduma nyingine kwa jamii kutokana na matumizi yake kukua kwa kasi.
Teknolojia imekuwa rasilimali muhimu ya maendeleo na chanzo kikubwa cha ushindani wa sekta mbalimbali.
Kila sekta ikiwamo ya elimu inahangaika kuona inabuni mbinu mbalimbali ilimradi kwenda sambamba na ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TATAKI), ni miongoni mwa taasisi zilizoamua kuja na teknolojia mpya ya kupakia kamusi ya Kiswahili kwenye simu ya kiganjani.
Katika maonyesho ya Wiki ya Tafiti ya UDSM, jijini Dar es Salaam, teknolojia hiyo ilikuwa ni miongoni mwa tafiti zilizowavutia wengi kutokana na umuhimu wa kamusi katika kukuza lugha ya Kiswahili.
Mtaalamu wa kamusi hiyo, Dk George Mrikalia anasema yapo matumizi mengi ya siku za mkononi ikiwamo kupashana habari, lakini kuwapo kwa kamusi ni aina mpya ya matumizi.
Mkuu wa Tafiti wa UDSM, Profesa Cathbert Kimambo anasema inawezekana kuifikia Tanzania ya viwanda haraka, ikiwa kila sekta itatoa tafiti zenye lengo la kutambua changamoto za jamii na kutoa suluhisho la namna ya kuondokana nazo.
Kutokuwa na kamusi ya Kiswahili kwenye simu ni kati ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumiaji wengi wa lugha hiyo. Lakini sasa changamoto hiyo imefikia tamati.
Dk Mrikalia anasema siyo tu kamusi hiyo itaongeza kasi ya kukua kwa lugha ya Kiswahili duniani kwa kuwa mtumiaji ataweza kupata tafsiri ya maneno anayohitaji mahali popote, bali itakuwa njia rahisi ya watu kujifunza hasa shuleni na vyuoni.
Wageni kunufaika
Dk Mrikalia anaeleza kuwa watumiaji wengi wakiwamo wageni wanaopenda kujifunza Kiswahili wataweza kuipata kwa haraka zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna baadhi ya mataifa, sio rahisi kukutana na kitabu cha kamusi ya Kiswahili dukani.
“Hakuna sababu za kuhangaika tena kwa sababu kila kilichokuwa kwenye kitabu kimehamishiwa kwenye simu,”anasema.
Mhadhiri Mwingine wa Chuo hicho, Dk Shani Omary anasema ukweli ni kwamba, hakuna anayeweza kukataa mabadiliko, hivyo wamelazimika kuja na kamusi hiyo kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Anasema wakati mwingine, huwawia vizumu zaidi baadhi ya watumiaji Kiswahili kutafuta kamusi za vitabu madukani kutokana na kubanwa na muda.
“Nasi wataalamu wa lugha tumekumbwa na ulimwengu wa sayansi na teknolojia, siyo rahisi kukimbia kwa sababu watumiaji wanahitaji mabadiliko. Hivi sasa popote mtu anaweza kuipata, siyo lazima aende dukani hivyo mbio za sayansi na teknolojia zimetulazimisha kufanya mradi huu wa kamusi ya Kiswahili, kwenye simu ya mkononi,”anasema.
Kilichomo kwenye kamusi
Hakuna kitu kizuri kama kutumia misemo, tamathali za semi na methali unapofikisha ujumbe.
Dk Mrikalia anasema wamefanikiwa kupakia kwenye simu vitu vyote vya muhimu ambavyo watumiaji wa lugha wanahitaji na kwamba, itakuwa rahisi kwa watumia kujua mambo mengi zaidi kuhusu lugha ya Kiswahili.
“Ni kamusi ya Kiswahili kwenda Kiingrereza na Kiingereza kwa Kiswahili; itawasaidia watumiaji wa lugha ya Kiswahili ambao huhangaika kila uchao kutafuta maana ya maneno,” anasema.
Mtumiaji atalazimika kupakua kwenye simu yake baada ya kuilipia kupitia huduma za kifedha za kwenye simu.
“Ukilipia mara moja na ikaingia kwenye simu yako, utaendelea kuitumia moja kwa moja kwa maana nyingine, haihitaji kuwapo kwa mtandao,” anasema.
Jinsi ya kuipata
Dk Mrikalia anasema kwa kuanza, watumiaji wataweza kuinunua kamusi hiyo kwa njia ya Mpesa na kwamba, wanatarajia kuzundua Juni mwaka huu.
“Tupo kwenye hatua za mwisho za kuingia mkataba na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom; mtumiaji atatakiwa kulipia kwa Mpesa kisha atapewa namba ya siri na hapo ataweza kuipakua kamusi yake,” anafafanua.
Anasema mtumiaji akishalipia mara moja na kupakua kwenye simu yake, kitakachobaki ni matumizi tu.
Anaeleza kuwa inapotokea siku imeibiwa, mtumiaji anaweza kuipakua kamusi nyingine kwenye simu yake mpya kwa kutumia namba za awali, kisha ile iliyo kwenye simu iliyoibiwa itapotea.







Previous
Next Post »