FRIJI LATEKETEZA JENGO LA GHOROFA 27 KWA MUDA WA DAKIKA 15 - Rhevan Media

FRIJI LATEKETEZA JENGO LA GHOROFA 27 KWA MUDA WA DAKIKA 15


MOTO uliozuka kwenye jengo la ghorofa 27 lililoko London Magharibi kwa dakika 15 baada ya friji kulipuka, itakuwa ni moja ya ajali mbaya kupata kutokea katika historia ya nchi hii huku kukiwa na hofu ya kutokuwa na manusura katika ghorofa tatu za juu.

Watu sita wamethibitishwa kupoteza maisha katika moto huo ulioligubika jengo la Grenfell Tower lililoko White City, ulioanza baada ya saa saba usiku wa kuamkia jana, lakini kikosi cha upelelezi cha Scotland Yard kilisema jana kuwa idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Kiongozi wa eneo hilo ambaye anashiriki kutambua waliko waathirika, na ambaye hakutaka kutajwa jina, anaamini kwamba hakuna mtu anayeishi katika ghorofa tatu za juu aliyesalimika na jengo hilo linaweza kuporomoka ndani ya saa 24 zijazo.

Alisema: “Tuna orodha ya watu waliopotea – ni wengi. Inawezekana wako wengi zaidi ya 50, pengine hata mamia.” 

Walioweza kukimbia walisema ndani ilikuwa sawa na “jehanamu duniani” wakati wakikanyaga miili na kudai kukosekana kwa ving’ora vya moto huku njia pekee ya kutokea nje ikijifunga.

Kutokana na taharuki hiyo, wakazi wa jengo hilo walionekana wakijirusha na kurusha watoto wao kupitia madirishani, kuchelea kufa kwa kuunguzwa na moto-wengine walitengeneza kamba kwa kutumia mashuka au kuzitumia kama parachuti na kujirusha.

Baraza la mtaa, mmiliki wa jengo hilo na mjenzi walikuwa wakilifanyia matengenezo mwaka jana, walikabiliwa na maswali mazito juu ya jinsi moto huo ulivyopamba haraka na kwa kasi katika jengo hilo lililopachikwa jina la ‘mtego wa kifo’ na walionusurika.
  
Huku kukiwa bado na hofu ya vifo zaidi, ilibainika kuwa waliokufa ni sita huku wengine 74 wakilazwa kwenye hospitali sita za hapa wakiwamo 20 walio katika hali mbaya.

Wazimamoto 200 na mashine 40 za kuzimia moto zilitakiwa ili kukabiliana nao.

Wakazi hao walishalalamika huko nyuma, kuhusu usalama wa moto katika jengo hilo kwa mmiliki wake, Shirika la Usimamizi wa Wapangaji la Kensington and Chelsea (KCTMO), lakini malalamiko yao yakagonga ukuta.
Previous
Next Post »