Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imesifu hatua za awali zilizochokuliwa na Rais John Magufuli katika kupambana na rushwa, na imeipa Serikali njia tano zitakazoongeza ufanisi katika vita hiyo badala ya kutegemea kuboresho sheria au kuwaanika hadharani watu waliokutwa na kashfa za ufisadi.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird alisema jana kuwa benki hiyo imejiridhisha kuwa mafanikio katika vita dhidi ya rushwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi inayopambana na umaskini.
Bird aliwaeleza wajumbe wa mkutano wa kimataifa wa maboresho ya vita dhidi ya rushwa kuwa kwa miaka 20 waliyoshirikiana na nchi mbalimbali duniani kupambana na vitendo hivyo, wamejifunza mengi na somo la kwanza ni katika vita hiyo, Serikali inatakiwa kuhakikisha inaboresha motisha kwa wafanyakazi wake.
Alisema mawaziri na watu wengine wanaoshughulikia ukusanyaji wa kodi au kufundisha watoto, hawaishii tu kufuata sheria na kanuni hususan pale zinapowataka wafanye mambo magumu au kurudisha fedha wanazokuwa wamezipata, “Vita dhidi ya rushwa inamalizwa kwa kuandaa mfumo wa hatua zinazozingatia maadili, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa vitendo vya maofisa na kuadhibu kwa tabia zinazoenda kinyume,” alisema.
Bird alisema somo la pili walilojifunza ni kuwa, uzuiaji wa rushwa ni muhimu katika vita hiyo.
Alisema licha ya ukweli kuwa polisi, waendesha mashtaka na majaji wana mchango mkubwa katika kutokomeza vitendo hivyo, hakuna nchi iliyofanikiwa kwa kusisitiza kuwashtaki mafisadi peke yao.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Bird alisema rushwa inazuiwa wakati sheria na utaratibu uko wazi na maofisa wameshapatiwa mafunzo ya namna ya kufanya kazi na mifumo ipo tayari kuwafuatilia na kuchukua hatua.
“Vita ya rushwa katika baadhi ya maeneo, haipunguzi bali inahamisha vitendo hivyo. Mfano nchi nyingi zilijikuta zikitumia nguvu nyingi kupunguza rushwa kwenye utoaji wa zabuni, baadaye wakagundua ufisadi umehamia kwenye utekelezaji wa kandarasi hizo,” alisema.
Katika jambo la nne, Bird alisema ili kuondoa ufisadi, unahitajika muungano wa watu na taasisi za umma, asasi za kiraia na sekta binafsi, kwa kuwa vita hiyo inahusisha namna Serikali inavyoshirikiana na wadau hao.
Katika njia ya tano, mama huyo alisema vita ya rushwa inahitaji jitihada za muda mrefu na zinazobadilika mara kwa mara ili kuendana na wakati.
Alisema WB iko tayari kuisaidia Tanzania kupunguza ufisadi ili kuboresha utoaji wa huduma bora zitakazong’arisha maisha ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema kukithiri kwa rushwa nchini kumewafanya wananchi kuichukia Serikali na kwamba imejidhatiti vilivyo kuendelea kupambana na janga hilo kwa nguvu zake zote. Alisema rushwa hufanyika kwa siri hivyo mapambano yake yanahitaji ushirikiano mkubwa baina ya Serikali, wadau wengine na wananchi katika kuitokomeza.
“Serikali yetu chini ya Rais John Magufuli imepania kupambana na rushwa kwa namna yoyote ile na tayari ipo mikakati tuliyoiweka kwa ajili ya suala hili.”
Sign up here with your email