KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli usiku huu baada ya kuichapa Mbao mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Azam FC kuzidi kujikita katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 49 na kuiacha Kagera Sugar chini yake iliyofikisha 47 kufuatia sare ya 1-1 waliyoipata dhidi ya Ruvu Shooting lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Kabla ya kuanza mchezo huo, timu zote mbili zilisimama kimya kwa dakika moja na huku Azam FC ikivaa vitamba vyeusi begani kuomboleza vifo vya wanafunzi 32 wa Shule ya Lucky Vincent iliyoko eneo la kwa Mrombo, waliofariki leo kwenye ajali ya basi aina ya costa lililotumbukia katika Mto Marera ulioko katika Mlima Rhotia, Karatu mkoani Arusha.
Azam FC inaungana na Watanzania wote kuomboleza vifo hivyo na tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia za wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na athari za ajali hiyo.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu, walifanikiwa kumiliki asilimia kubwa na mchezo siku ya leo wakicheza kwa soka la kitabuni la pasi, jambo ambalo liliwapoteza wapinzani wao na kujikuta wakiruhusu mashambulizi mengi langoni mwao.
Shukrani kwa mabao safi yaliyowekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyefunga la kwanza kwa ustadi mkubwa dakika ya 13, huku Shaaban akitupia mengine mawili kipindi cha pili dakika ya 53 na 59 na kuhitimisha ushindi huo mkubwa wa Azam FC.
Bao alilofunga Bocco linamfanya kufikisha mabao tisa msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) huku Shaaban aliyeingia dakika ya 29 kuchukua nafasi yanaye akiwa nayo sita kwenye ligi hiyo.
Bao pekee la Mbao limewekwa kimiani na Ndaki Robert dakika ya 84.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameweza kuituliza Mbao kupitia mfumo wake wa 3-4-3 alioutumia leo, akiwategemea mabeki watatu wa kati, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris na Daniel Amoah kwenye eneo la ulinzi huku mabeki wa pembeni Bruce Kangwa na Shomari Kapombe, wakisaidia kwenye ulinzi na ushambuliaji,
Eneo la kiungo lilimilikiwa vema na Stephan Kingue, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Domayo kabla ya kuumia, ambao walikuwa wakiongezewa nguvu na mabeki wa pembeni na viungo washambuliaji Ramadhan Singano ‘Messi’ na Shaaban, wote wakicheza nyuma ya mshambuliaji mmoja Bocco.
Kikosi cha Azam FC:
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Stephan Kingue, Frank Domayo/Shaaban dk 29, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Mudathir Yahya dk 76, John Bocco (c)/Masoud Abdallah dk 85
Sign up here with your email