WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR KUPEWA MAFUNZO - Rhevan Media

WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR KUPEWA MAFUNZO

ZAB

Serikali imeshauriwa  kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari ili waandishi waweze kupata nafasi ya kufichua matatizo  yanayoikabili jamii na kupatiwa ufumbuzi.
Hayo yamesemwa leo huko Park Hyyat Hotel na mwandishi wa habari kutoka ubalozi wa Marekani nchini Tanzania  Kenneth Cooper wakati alipokuwa akitoa mafunzo kwa wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa nchini.
Amesema kuvitisha vyombo vya habari na kuvibinya katika kutekeleza majukumu yake ni kuvipotezea ufanisi na kupelekea kufanya kazi zake kwa woga na kushindwa kufichua maovu.
“Serikali ikubali na iheshimu uwepo vyombo vya habari, kwani kuvibinya nikusababisha matatizo nchini,” alisisitiza Kenneth Cooper.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa jamii kwani vinaweza kuibua matatizo yanayoikabili hivyo kupitia vyombo hivyo yanaweza kufika kwa wahusika.
Akizungumzia njia bora kwa  waandishi kutafuta na kuripoti habari, Cooper alisema mwandishi anatakiwa kuwa makini na mdadisi katika utafutaji wa habari.
Amewaeleza washiriki wa mafunzo kuwa wanapaswa  kujenga uhusiano mzuri na vyanzo vya habari ili  waweze kupata habari kwa urahisi  pamoja na kufuatilia mtiririko wa matukio mbalimbali,
Aidha amewahimiza waandishi kufanya utafiti na kutotosheka na chanzo kimoja cha habari  na kuweka umuhimu wa kutoa nafasi sawa kwa watu watakaohusika katika habari ili kuepuka matatizo .
Hata hivyo amesisitiza waandishi kufanya tathmini  na kujua thamani ya maisha yao ili kuweza kujali usalama wa maisha, kuweka matarajio ya kazi zao pamoja na kuwa na mashirikiano na waandishi wengine katika kutekeleza majukumu yao.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) Abdalla Abdulrahman Mfaume ameushukuru Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa kuwapatia mafunzo hayo jambo ambalo litawajengea uwezo na ameushauri ubalozi huo kuendelea kushirikiana na waandishi wa Zanzibar kwa mafunzo zaidi.
Previous
Next Post »