UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2016/17 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2017/18. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya mapato na Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo wa Wizara kwa mwaka 2017/18.
- Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa, napenda kuchukua fursa hii kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake imara kwa nchi yetu na maelekezo yake ambayo yamekuwa dira sahihi katika utendaji wangu na katika kuimarisha huduma za Afya na ustawi wa jamii nchini. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweka chachu katika kudhibiti matumizi ya madawa ya kulevya nchini ikiwa ni jitihada zake za kulinda afya za Watanzania hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa letu. Kwa hali hiyo, Wizara yangu itaendelea kuelimisha na kuhimiza umma wa Watanzania kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa ya kulevya.
- Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo na ushauri wake wa dhati hasa katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na masuala ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Wizara yangu itaendelea kutumia taswira, ushawishi na uzoefu wake ili kujenga jamii ya watanzania inayowajali, kuwaheshimu na kuwaendeleza wanawake na wasichana.
- Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake ambao umesaidia kuongeza ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma zinazotolewa na Wizara yangu. Aidha, naomba nimpongeze kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwenye Bunge hili ambayo imetoa dira ya jinsi Serikali itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2017/18.
- Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi, kwa kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa weledi katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nampongeza Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.) na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mijadala ndani ya Bunge.
- Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb) Waziri wa Nchi, OR- TAMISEMI kwa ushirikiano wake uliowezesha kusimamia na kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini hasa afya ya msingi. Pia, nawashukuru Mawaziri wa Wizara nyingine zote ambazo ushirikiano wao na Wizara yangu umechangia katika utoaji wa huduma za afya na maendeleo ya jamii.
- Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba (Mb), na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii nchini. Ninawashukuru sana!
- Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa wote walioteuliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha 2016/17. Ninawaahidi kuwapa ushirikiano ili tuendelee kuwatumikia wananchi kwa pamoja.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako, Bunge lako Tukufu, kwa familia na wananchi wa Jimbo la Dimani kwa kifo cha Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir na Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, CHADEMA. Aidha, natoa pole kwa watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu na jamaa zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa, ajali na majanga. Pia, natoa pole kwa wagonjwa na majeruhi wa ajali waliopo hospitalini na majumbani pamoja na wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Namuomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka ili waweze kuendelea na ujenzi wa Taifa.
- Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2016/17, Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2017/18 pamoja na maombi ya fedha ambazo zitaiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.
II: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NAMPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara imeendelea kuzingatia Sera, Mipango na Mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (2030), Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa II wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21), Sera ya Afya (2007), Mpango Mkakati wa IV wa Sekta ya Afya (2016 -2020) na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM 2007 – 2017). Aidha tumezingatia Sera ya Taifa ya Wazee (2003), Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996), Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2001). Vilevile, Wizara imeendelea kutekeleza malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.
Mapato na Matumizi ya Fedha – Fungu 52 (Afya)
- Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi 2017, Wizara kupitia Fungu 52 imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 118.7 sawa na asilimia 75 ya makadirio ya Shilingi bilioni 157.7 yaliyoidhinishwa kwa mwaka 2016/17. Usimamizi thabiti pamoja na matumizi ya mifumo ya Kielektroniki vimechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ufanisi huu.
- Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi, 2017, jumla ya Shilingi bilioni 339.1 zilipokelewa ikiwa ni asilimia 43 ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara.(Shilingi bilioni 1). Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 205.3 sawa naasilimia 74 ni fedha za Matumizi ya Kawaida ikiwemo Mishahara na Shilingi 133.8 sawa na asilimia 26 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Aidha, tumepokea vifaa, vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Shilingi 256,238,088,964.00 kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maendeleo.
Fungu 53 – Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
- Mheshimiwa Spika, kupitia Fungu 53 Wizara ilitarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni3. Vyanzo vya mapato ikiwa ni ada za wanafunzi katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na ada za Mashirika Yasio ya Kiserikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017, makusanyo yalifikia Shilingi 930,281,152 sawa naasilimia 39.0.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, jumla ya Shilingi 49,857,955,920 ziliidhinishwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara kupitia Fungu hili. Hadi kufikia mwezi Machi, fedha za Matumizi Mengineyo Shilingi 4,950,097,864 zilipokelewa sawa na asilimia 4 ya bajeti iliyoidhinishwa na Shilingi 7,866,426,933 za Mishahara zilipokelewa sawa na asilimia 42.1 ya bajeti iliyoidhinishwa. Vilevile, katika bajeti ya miradi ya Maendeleo, Shilingi 497,718,250 zilipokelewa ambapo Shilingi 204,217,000.
- Mheshimiwa Spika, ifuatayo ni taarifa kuhusu majukumu yaliyotekelezwa na Wizara katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017;
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA SEKTA YA AFYA
HUDUMA ZA KINGA
Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Yasiyoyakuambukiza
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kinga nchini ambazo zinajumuisha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa yaliyokuwa hayapewa kipaumbele, huduma za uzazi na mtoto,lishe pamoja na utoaji wa elimu ya afya kwa umma. Katika kipindi cha 2016/17 Wizara kazi zilizotekelezwa ni pamoja na;
Huduma za Chanjo
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za Chanjo kulingana na Sera na Miongozo. Aidha, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha kwa ajili ya huduma za chanjo kwa watoto na makundi mengine kwa kununua na kusambaza chanjo katika Mikoa na Halmashauri zote nchini ambapo jumla ya Shilingi bilioni 18 zimetumika. Utoaji wa huduma za uhakika wa chanjo imewezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2016, ambapo tuliweza kuvuka lengo kwa kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 97.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imenunua magari 9 kwa ajili ya kuboresha huduma za usambazaji wa chanjo. Pia wizara ilinunua na kusambaza majokofu 317 ya kutunzia chanjo kwenye vituo vya huduma za afya nchini.
Usafi wa Mazingira
- Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuratibu awamu ya pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira (2016-2021) ambapo katika mwaka 2016/17, jumla ya kaya 391,937 zimejenga vyoo bora, kati ya hizi, kaya 320,894 zina sehemu maalum ya kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni. Katika kuongeza chachu ya ushindani katika kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira, Wizara iliendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira na kutoa zawadi mbalimbali kwa Halmashauri zilizofanya vyema. Katika mashindano hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe iliibuka mshindi wa jumla kitaifa na kukabidhiwa zawadi ya gari jipya aina ya Toyota Hardtop 4WD. Aidha, Wizara ilinunua na kugawa jumla ya pikipiki kwa Halmashauri 100 nchini hususani za vijijini.
Udhibiti wa Magonywa yaliyokuwa hayapewa kipaumbele
- Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Taifa ya Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewa kipaumble imeendea kugawa dawa za kingatiba za matende, mabusha, usubi, trakoma, kichocho na minyoo ktk Halmashauri 71 zenye maambukizi ambapo watu million 14.3 walifikiwa. Aidha upasuaji wa matende na mabusha bila malipo umefanywa kwa wagonjwa 805 katika Halmashauri za Temeke na Ilala na 100 katika Mkoa wa Mwanza.
Udhibiti wa Malaria
- Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na mapambano dhidi ya Malaria, Wizara imesambaza dawa za kutibu malaria na vipimo vya kupima malaria (mRDT) kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya dozi za dawa mseto (ALU) milioni 12.5 na Vitepe vya mRDT milioni 15.5 vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya huduma za afya nchini pamoja na kuhamasisha matumizi ya kipimo cha mRDT. Vile vile unyunyiziaji wa dawa ukoka umefanyika katika mikoa 4 ya Kanda ya Ziwa ambayo ina maambukizi makubwa zaidi ya malaria ambayo ni (Kagera, Mwanza, Mara na Geita). Pia kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu imetekelezwa katika Halmashauri ya Kilombero – Morogoro na Halmashauri zote za Mkoa wa DSM. Jumla ya vyandarua milioni 2.6 vilinunuliwa na kusambazwa katika Halmashauri hizo.
Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma
- Mheshimiwa Spika, huduma za kifua kikuu na Ukoma zimeendelea kuimarika nchini ambapo mafanikio makubwa yameendelea kupatikana. Kwa hivi sasa kiwango cha wagonjwa wanaotibiwa na kuponani asilimia 90 kati ya waliogunduliwa kuugua kifua kikuu.Wizara imeendelea kuboresha huduma za vipimo kwa kuimarisha maabara 4 za Kandaya Mbeya (Hospitali ya Rufaa Mbeya), Mwanza (Bugando Medical Centre), Dodoma (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa) na Kilimanjaro (Hospitali ya Kibong’oto) ambazo zimeweza kufunguliwa na kuanza kutoa huduma za uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu.Hapo awali huduma hii ilikuwa inapatikana katika maabara moja tu iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
- Mheshimiwa Spika, huduma za uchunguzi na matibabu yakifua kikuu sugu zimeimarishwa na kusogezwa karibu na wananchi kutoka Hospitali moja ya Kibongoto hadi Vituo 18 Aidha, shughuli mbalimbali za uelimishaji na uhamasishaji jamii kuhusu Kifua Kikuu zilitekelezwa ikiwemo kuendesha Kampeni kupitia vyombo vya habari (TV, Radio) yenye lengo la kuibua wagonjwa wapya wa kifua kikuu kwa kuwa ni asilimia 39 tu kati ya wagonjwa 162,000 waliopo nchini ndio walio katika matibabu.Tunamshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini. Nisisitize kuwa Kifua Kikuu Kinatibika na Huduma za Kupima na Matibabu hutolewa bila Malipo.
Udhibiti wa UKIMWI
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti UKIMWI kwa kutoa ushauri nasaha na kupima virusi vya UKIMWI (VVU) pamoja na kutoa dawa za watu wenye maambukizi ya Virusi vya VVU/UKIMWI (WAVIU). Kuanzia mwezi Januari hadi Desemba, 2016 jumla ya wateja wapya milioni 7.4 walipata ushauri nasaha na kupima VVU.
- Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Oktoba 2016, Wizara ilianza kutoa dawa za ARV kwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya VVU/UKIMWI (WAVIU) bila kujali kiwango cha CD4 ambapo hadi Machi 2017 jumla ya WAVIU wanaotumia ART/ARV ni 849,594 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya watu million 1.4 wanaokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU nchini. Kati ya hao watoto 55,670 wako kwenye matibabu ya ARV. Pia, Wizara imefunga mashine mpya 14 za kupima uwingi wa virusi vya UKIMWI (viral load) katika damu katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mtwara, Dodoma, Tabora, Iringa, Morogoro, Arusha, Ruvuma, Kagera na Rukwa na Hospitali za Rufaa za Kanda – Bugando, Mbeya, KCMC, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Maabara ya Taifa ya Viwango na Ubora.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza afua ya tohara kwa wanaume kama mojawapo ya afua ya kupambana na maambukizi ya VVU. Kuanzia mwezi Januari hadi Desemba, 2016 jumla ya wanaume 374,411 kati ya lengo la wanaume 492,844 wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 49 wamepata huduma ya Tohara kutoka mikoa 14 ya kipaumbele.
Udhibiti wa Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza
- Mheshimiwa Spika; kutokana na ongezeko kubwa la Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile Kisukari, Shinikizo la Damu na Magonjwa ya Moyo, Wizara imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa 2016 – 2020 ambao ulizinduliwa Dodoma mwezi Novemba 2016. Hatua hiyo ilifuatiwa nakuanzishwa kwa Kampeni ya Kitaifa inayolenga katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa. Kampeni hiyo ilizinduliwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan mwezi Desemba 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Makamu wa Rais aliagiza kuwa kila Jumamosi ya Pili ya Mwezi iwe ni Siku ya Hamasa ya Kufanya Mazoezi. Afya Yako Mtaji Wako
- Aidha Wizara iliendelea na jitahada mbalimbali zenye lengo la kuelimisha jamii juu ya madhara ya Tumbaku. Kuanzia Januari 2017, Kanuni za Kudhibiti Tumbaku zinataka maandishi ya onyo “uvutaji wa Sigara una madhara” yawe yenye ukubwa wa asilimia 30 ili yaweze kuonekana mazuri
Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto
- Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa huduma inayofikiwa na wanawake wote, kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, na wakati wa kujifungua hadi wiki sita baada ya kujifungua ni muhimili muhimu wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Hata hivyo, tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto. Tafiti zilizofanyika hapa nchini mwaka 2015 zinaonyesha kwamba idadi ya vifo ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Katika kuimarisha huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini, Wizara imeandaa Mpango Mkakati wa miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na vijana pamoja na mambo mengine kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020. Katika kutekeleza mkakati huo, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu: ambayo ni:huduma ya uzazi wa mpango,huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua.
- Mheshimiwa Spika, kuhusu huduma za uzazi wa mpango, Wizara imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana kwa wote wanaoihitaji. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya wateja 357,244 walifikiwa kupitia huduma za mkoba na 2,509,280 walifikiwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya. Wizara imenunua na kusambaza dawa za uzazi wa mpango.Utekelezaji wa afua hizo umewezesha kiwango cha kutumia uzazi wa mpango kupanda kutoka asilimia 27 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2015/16 (TDHS, 2015). Lengo ni kufikia asilimia 45 mwaka 2020.
- Mheshimiwa Spika, imebainika kuwa matatizo mengi wakati wa ujauzito yanaweza kuzuilika, kugundulika na kutibiwa kama wanawake wajawazito watahudhuria kliniki ya wajawazito na kupimwa na wahudumu wenye ujuzi. Katika kipindi cha 2016/17, Wizara iliendelea kuhakikisha huduma kwa wanawake wajawazitozinapatikana sambamba na kuelimisha wajawazito kuhudhuria kliniki.Kulingana na tafiti zilizofanyika mwaka 2015/16 asilimia 98 ya wajawazito wote walihudhuria kliniki angalau mara moja na asilimia 51 walihudhuria angalau mara 4 ambacho ni kiwango cha chini cha mahudhurio kinachopendekezwa. Lengo ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara 4 katika kipindi cha ujauzito ifikapo mwaka 2020. Nitumie fursa hii kuwahimiza akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito wao ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi vinavyoepukika.
- Mheshimiwa Spika, upatikanaji wahuduma wakati wa kujifungua ikiwemo huduma ya dharura wakati wa kujifungua hadi wiki sita baada ya kujifungua, ni muhimu sana ili kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi. Huduma kwa matatizo haya hupatikana tu kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya na mtoa huduma mwenye ujuzi. Katika mwaka 2016/17, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhamasisha na kuhimiza wanawake wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma.Idadi ya akinamama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 64 mwaka 2015/16. Napenda kutoa wito kwa wanawake wajawazito wote nchini wajifungulie kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupunguza vifo na changamoto za uzazi kwa mama na mtoto.
- Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI, imekamilisha ukarabati wa vituo vya afya 8 katika Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu na Mara ili kusogeza huduma karibu na wananchi za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni (CEmONC). Hadi sasa, Kati ya Vituo vya Afya 473 vinavyomilikiwa na Serikali ni vituo vya Afya 117sawa na asilimia 21 ndio vinatoa huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni.Lengo la serikali ni kuhakikisha angalau asilimia50 ya vituo vya afya nchini vinatoa huduma kamili za uzazi wa dharura ifikapo mwaka 2020.
- Mheshimiwa Spika, Huduma za Rufaa kwa Wajawazito zimeendelea kuboreshwa ambapo Wizara imegawa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) 67 katika Halmashauri za Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na Kigoma na mikoa mingine hapa nchini. Aidha, Wizara imegawa magari 8 kwa ajili ya kuratibu shughuli za afya ya mama na mtoto katika Kanda ya Ziwa, Kati, Magharibi, OR – TAMISEMI Dodoma, na magari 2 katika kitengo cha Afya ya mama na Mtoto Wizarani. Hatua hiyo itatoa msukumo na kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika mikoa hiyo ambayo takwimu zimeonesha kuwa wana vifo vingi zaidi.
- Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua hatua kwa ajili ya kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kutaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kijadiliwe ndani ya saa 24 katika kituo/hospitali husika kwa lengo la kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuboreshwa zaidi kwa huduma zinazotolewa katika kituo husika. Sambamba na hilo Wizara kuanzia mwezi Oktoba 2016 imeanzisha utaratibu wakutaka kila halmashauri na mikoa nchini kutoa taarifa ya vifo vitokanavyo na uzazi kila mwezi.
- Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu tumeeleza hatua tulizochukua ili kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 ikiwemo watoto wa chini ya mwezi mmoja vipungue kutoka 21 hadi 16 katika kila vizazi hai 1,000; vifo vya watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kutoka 45 hadi 25 katika kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka 54 hadi 40 katika kila vizazi hai 1,000
Huduma za Lishe
- Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na asasi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali kuhamasisha masuala ya Lishe sambamba na kuhakikisha virutubishi muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili vinaendelea kupatikana kote nchini. Kwa sasa urutubishaji unaoendelea ni ule wa uongezaji wa virutubishi muhimu kwenye unga wa mahindi na usindikaji wa mafuta ya alizeti kwa kuongeza vitamini A. Aidha kupitia mpango wa urutubishaji chakula kwa kutumia virutubishi nyongeza kwenye chakula cha kawaida kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59 katika ngazi ya jamii (Home food Fortification) umefanyika ktk mikoa mbalimbali nchini.
HUDUMA ZA TIBA
Huduma za Damu Salama
- Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama imeendelea kutekeleza jukumu la ukusanyaji na usambazaji wa Damu Salama nchini, ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya chupa za damu 145,300 zilikusanywa, sawa na asilimia 63 ya lengo la kukusanya chupa 230,000 kwa mwaka. Chupa zote za damu zilizokusanywa ziliweza kupimwa ambapo na asilimia 90 ya chupa za damu zilizokusanywa zilionekana kutokuwa na maambukizi ya aina yoyote na hatimaye kusambazwa hospitalini kwa ajili ya kupewa wagonjwa wahitaji.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanzisha utaratibu wa kuwa na vituo vya benki za damu kwenye ngazi ya mikoa ili visaidiane na benki za damu za kanda katika kuboresha upatikanaji wa damu salama hususani kwa akina mama wajawazito. Hadi sasa Benki za damu za Mikoa 7 zimeanzishwa katika mikoa ya Dar es salaam, Lindi, Morogoro, Dodoma, Iringa, Kigoma na Shinyanga. Uanzishwaji wa benki hizo katika mikoa ya Mara na Kagera upo katika hatua za mwisho. Lengo ni kuhakikisha kila Mkoa una Benki ya Damu ikiwa ni jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Huduma za Maabara za Uchunguzi wa Magonjwa
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha huduma za maabara za uchunguzi wa magonjwa ya binadamu ikiwemo Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (kama nilivyoeleza katika aya ya 56 ya Hotuba yangu.
Upatikanaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika mwaka 2016/17, Wizara ilitenga Shilingi bilioni 251.5 kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba,na vitendanishi ikilinganishwa na kiasi cha Shilingibilioni 31kilichotengwamwaka 2015/16. Hadi kufikia Machi 2017, jumla ya Shilingi bilioni 112.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 24 zilizotolewa mwaka 2015/16.Hadi kufikia mwezi Machi 2017 mikoa/halmashauri/hospitali zimepokea zaidi ya asilimia 95.
- Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi, 2017, asilimia 81 ya dawa muhimu zaidi (essential medicine) zinapatikana katika Bohari ya Dawa. Ongezeko hili la upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 36 kipindi cha mwezi Juni 2016 na kufikia asilimia 81 mwezi Machi, 2017 limetokana na uamuzi wa Serikali wa kuongeza bajeti ya dawa na kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya dawa,vifaa, vifaa tiba, na vitendanishi. Aidha, Wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo ununuzi wa dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama za dawa na kuongeza uwezo wa MSD kununua dawa nyingi zaidi.Lengo la Wizara ni kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inafikia asilimia 90 ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha 2016/17.
- Mheshimiwa Spika, Wizara pia imetekeleza ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya cha umma kinakuwa na vifaa vya kutosha. Katika mwaka 2016/17, Wizara imenunua na kuanza kusambaza kwa kila Halmashauri vitanda vya kawaida 20, vitanda vya kujifungulia 5, magodoro 25 na mashuka 50.Uzinduzi wa zoezi hili umefanyika mwezi Aprili 2017 katika halmashauri ya Kongwa Dodoma. Jumla ya vitanda vya kawaida (Hospital beds) 3,680, vitanda vya kujifungulia (delivery beds) 920, magodoro 4,600 na mashuka 9,200 vimenunuliwa ambapo thamani yake ni Shilingi bilioni 2.9.
Uimarishaji wa Huduma za Matibabu ya kibingwa
- Mheshimiwa Spika, moja ya jukumu la kipaumbele kwa Wizara ilikuwa ni kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za kibingwa zitolewazo nchini. Maboresho hayo, yanalenga katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo serikali inaingia katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Hadi kufikia Machi 2017, idadi ya Wagonjwa waliopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ilipungua kwaasilimia 35 kutoka wagonjwa 553 mwaka 2015/16 hadi Wagonjwa 357 mwaka 2016/17.Mafanikio haya ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Hospitali zilizo chini ya Wizara zinazotoa huduma za Kibingwa ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), MOI na Ocean Road.
Hospitali ya Taifa Muhimbili
- Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Taifa Muhimbili imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji wahuduma za kibingwa. Hatua hizo ni pamoja na kufanya ukarabati wa Wodi 5 za wagonjwa mahututi (ICU).Ukarabati huo utaongeza vitanda vya ICU kutoka 21 na kufikia 75. Aidha, Hospitali imeanza kukarabati jengo kuu la upasuaji wa kina mama wajawazito na jengo la upasuaji wa watoto; ukarabati huo utaongeza vyumba vya upasuaji 6 na na kufikia jumla ya vyumba 19. Upanuzi wa jengo la kusafisha figo unafanyika ambao utaongeza vitanda 27 na kufikia jumla ya vitanda 42.
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya MOI imeendelea na juhudi za kupanua wigo wa huduma huduma ya upasuaji wa mifupa ikiwemoe migongo ya watoto iliyopinda.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya MOI kwa kushirikiana na GSM Foundation imetoa huduma ya upasuaji wa vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watotokupitia kambi Tiba katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na hospitali ya Mnazi Mmoja – Zanzibar. Katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017, jumla ya watoto 2,200 walifanyiwa uchunguzi na watoto 250 walifanyiwa upasuaji kwa mafanikio na kutoa mafunzo kwa Madaktari wa upasuaji katika hospitali za rufaa za mikoa/kanda nchini.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI)
- Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Julai 2016 hadi 2017, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKC) imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo ikiwemo kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 236, idadi hii ni sawa na wastani wa wagonjwa 30 kwa mwezi ukilinganisha na wastani wa wagonjwa 15 kwa mwezi katika mwaka wa fedha 2015/16. Aidha jumla ya wagonjwa 608 walipatiwa matibabu maalum kupitia tundu dogo kwa kutumia mtambo wa kisasa – catheterization laboratory (stents, percutaneous intervention, device closure, pacemarker). Idadi hii ni ongezeko la asilimia 190 ukilinganisha na wagonjwa 290 waliohudumiwa katika mwaka wa fedha 2015/16. Vile vile iliendesha kambi 3 za upasuaji kwa kushirikiana na mataifa rafiki (Israel, Germany na Australia). Hatua hiyo imesaidia kujenga uwezowa madaktari wazawa kwa kupata utaalam wa kupasua wagonjwa kutumia tundu dogo.
Taasisi ya Saratani OceanRoad
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani Ocean Road imehudumia wagonjwa wa Saratani nawagonjwa wasio wa saratani kama nilivyoeleza kwenye aya ya 75 hadi 79 ya Hotuba yangu. Masuala makubwa ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa jengo la kutolea tiba ya dawa (chemotherapy) pamoja na kununua vifaa na vitanda ambapo idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa imeongezeka kutoka wastani wa wagonjwa 40 hadi kufikia wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.
- Aidha, Taasisi imeweza kupunguza muda wa kusubiri kuanza tiba za mionzi (radiotherapy) kutoka miezi 3 hadi wiki 6; kwa kuhakikisha wagonjwa wanapata tiba mara mbili kwa wiki na kufanya matengenezo ya mashine kwa haraka. Lengo la Wizarani kupunguza muda huo uwe chini yawiki 2 pindi mashine mpya za LINAC zitakaposimikwa.
- Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa dawa za saratani umeboreshwa kutoka asilimia 4 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 60 mwezi Machi, 2017; na kwa baadhi ya saratani kama ya mlango wa kizazi, saratani ya koo na tezi dume dawa za dripu (chemotherapy) zinapatikana kwa asilimia 100.
- Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani OceanRoad ilikamilisha ujenzi wa jengo la ‘bunker’ ambapo mashine za mionzi za LINAC pamoja na CT Simulator zitasimikwa.
Hospitali Maalumu ya Kibong’oto
- Mheshimiwa Spika, Hospitali iliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu na UKIMWI, Kifua Kikuu Sugu na Kifua Kikuu cha kawaida (aya ya hotuba yangu). Aidha hospitali imepata mashine ya kupima usugu wa vimelea vya Kifua Kikuu kwa dawa daraja la pili na kupunguza muda wa uchunguzi wa Kifua Kikuu Sugu Zaidi (Extensive drug Resistant TB) chini ya siku 90. Pia hospitali imeweza kufupisha muda wa kuanza Tiba kutoka siku 14 mpaka siku 3 tangu mgonjwa kugundulika kuwa na kifua Kikuu Sugu hivyo kupunguza maambukizi kwa jamii.
Hospitali ya Mirembe
- Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Mirembe ilihudumia wagonjwa wa akili na magonjwa ya kawaida wakiwemo wagonjwa wa akili wahalifu.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya)
- Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Mbeya imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wagonjwa waliolazwa. Aidha, Hospitali imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa, ambapo hadi kufikia Machi 2017, jumla ya wagonjwa 37 walifanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.
- Mheshimiwa Spika, Hospitali pia imeendelea kuboresha na kupanua wigo wa huduma zinazotolewa kwa kukarabati jengo la daraja la kwanza na kukamilisha ujenzi wa jengo la watoto. Kukamilika kwa miradi hiyo miwili kutaongeza uwezo kwa hospitali kutoka vitanda 477 vya sasa mpaka vitanda 605.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Hospitali imeanzisha Idara ya matibabu ya pua, koo na masikio (ENT) na hivyo kuwaondolea wananchi wa Kanda hiyo usumbufu wa kusafiri kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hadi kufikia mwezi Machi 2017 wagonjwa 883 wenye matatizo hayo wamehudumiwa. Aidha, Idara ya Mifupa imeimarishwa baada ya kupata vifaa vya sign nailssets hivyo kupunguza muda wa wagonjwa walio vunjika kukaa wodini ambapo kwa sasa mgonjwa hukaa wodini kwa muda wa chini ya siku tatu ikilinganishwa na siku 42 ilivyokuwa hapo awal Vilevile, Huduma ya kusafisha figo (dialysis) imeimarishwa kwa kununua vitanda vipya 3 na hivyo kufikisha idadi ya vitanda 6.
Sign up here with your email