UONGOZI wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (Dorefa), umefurahia uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupeleka fainali za Kombe la FA katika Uwanja wa Jamhuri, imefahamika.
Fainali hizo za pili zitakazofanyika Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo zitaikutanisha Simba ya jijini Dar es Salaam na Mbao FC kutoka Mwanza.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema jana kuwa fainali hizo zimepelekwa Dodoma kutokana na Uwanja wa Taifa jijini utakuwa umefungwa ili kupisha ukarabati unaotakiwa kufanyika hasa kwenye eneo la kuchezea.
Malinzi alisema kuwa TFF imelazimika kuacha kuchagua uwanja utakaotumika kuchezewa fainali kwa mtindo wa droo kwa sababu ya kubaki na Uwanja wa CCM Kirumba peke yake ambao unatumiwa na Mbao FC.
"Napenda nitangaze kuwa fainali za Kombe la FA sasa zitafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, hii tumezingatia mambo mbalimbali hadi kufikia uamuzi huu," alisema Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA).
Mwenyekiti wa Dorefa, Mulamu Nghambi, aliliambia gazeti hili jana kuwa wamefurahia uamuzi huo na wataanza maandalizi ya mchezo huo mapema ili kuhakikisha fainali hizo zinachezwa katika kiwango cha juu.
"Tayari mkoa wetu ulikuwa katika programu za kualika timu mbalimbali kuja kucheza, tutaendelea pale tulipofika, napenda kuwahakikishia ulinzi na usalama pia utakuwa wa hali ya juu kwa mashabiki wote watakaofika hasa wa Simba ambao watatoka nje ya Dodoma," alisema Nghambi.
Mwenyekiti huyo alisema pia wataratibu usafiri kutoka wilaya zote za mkoa huo kwa ajili ya kurahisisha mashabiki kufika na kuondoka kwa urahisi uwanjani hapo.
Alisema pia uwanja huo unaingiza mashabiki wasiozidi 15,000 hivyo tiketi zitauzwa mapema ili kuondoa usumbufu.
Simba imetinga fainali hizo baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0 wakati Mbao FC iliwavua ubingwa Yanga kwa kuipa kichapo kama hicho, bao ambalo walijifunga kupitia kwa beki wao Andrew Vincent 'Dante'.
Sign up here with your email