LOWASSA ' AMNG'ATA SIKIO ' UHURU KENYATA - Rhevan Media

LOWASSA ' AMNG'ATA SIKIO ' UHURU KENYATA


Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemuonya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya dhidi ya muungano wa vyama vya upinzani wa Nasa, akisema utakisumbua chama tawala cha Jubilee katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti.
Akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Utangaza la Uingereza (BBC) juzi, licha ya kusisitiza msimamo wake wa kumuunga mkono Kenyatta kuwania urais kwa awamu ya pili, Lowassa alisema Nasa ni umoja ambao pia una nguvu.
“Nawapongeza Nasa kwa muungano wao. Namshauri rafiki yangu Kenyatta asipuuze muungano ule kwa sababu una nguvu, na una watu wengi. Naamini hatapuuza,” alisema Lowassa, ambaye pia aligombea urais nchini akiungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Lowassa alisema wakati mwingine chama kinapokuwa kimoja kura hazitoshi ndiyo maana vingine huungana kuwa kitu kimoja.
“Inawezekana mnapokuwa chama kimoja kura hazitoshi kwa hiyo mnajiunga na vyama vingine mnatengeneza ‘coalition’ na kama imejitengeneza vizuri mnachukua madaraka,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Niko upinzani kwa sababu maalumu ya kuing’oa CCM madarakani.”
Alipoulizwa kama Nasa wana nguvu ya kutosha ya kumng’oa Rais Kenyatta, alisema hana uhakika lakini nguvu ya muungano ni kubwa.
“Wapinzani wengi tutajifunza kutoka kwao kutokana na muungano huo hasa kama watafanikiwa.”
Licha ya kubashiri kuwepo kwa ushindani mkubwa, Lowassa aliwashauri Wakenya kuzingatia amani.
“Watangulize amani na umoja mbele wakati na baada ya uchaguzi,” alisema.
Kuhusu kumuunga mkono Kenyatta, Lowassa alisema: “Kwanza ni wakati wenyewe wa kura za maoni za vyama, pili namuamini mtu mwenyewe, na tatu nataka kauli yangu isikike. Jana (juzi) nilikuwa na wanawake wa Kenya na walifurahi sana kusikia namuunga mkono,” alisema Lowassa.
Lowassa alisema Rais Kenyatta amekuwa mmoja wa viongozi wanaoonekana kupenda na kuilinda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Tunataka viongozi wanaojali watu. Wakati EAC inaanzishwa tulikiri kwamba ni jumuiya ya watu na huyu ameonyesha kwamba hii ni jumuiya ya watu,” alisema.
Mbali na kumsifia, Lowassa pia alisema kwa kipindi ambacho Rais Kenyatta amekuwa madarakani, amefanya kazi nzuri na ameonyesha ana uwezo, anapenda amani na maendeleo .
Lowassa alishika nafasi ya pili katika mbio za urais Tanzania akiwa amepata kura milioni 6.07 huku Rais John Magufuli akipata milioni 8.8.     







Previous
Next Post »