JESHI STARS HAWASHIKIKI WAVU - Rhevan Media

JESHI STARS HAWASHIKIKI WAVU



TIMU ya Jeshi Stars (Wanaume) imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Wavu, Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA) kwa kuwatungua vijana wa Makongo seti 3-1, huku timu yao ya wanawake ikifungwa na Magereza.
Jeshi Stars wanaume ambao ni watetezi ikicheza bila nyota wao Nassoro Sharif ambaye nafasi yake ilizibwa vema na John Malumbu na Twalib Said iliwakimbiza Makongo na kupata ushindi huo uliowafanya wafikishe pointi 20.
Timu hiyo imekaa kileleni ikiwa haijapoteza mechi hata moja, huku ikisaliwa na michezo mitatu kabla ya kumaliza duru la kwanza na Kocha wa Makongo, Yusuf Mkarambati alikikubali kipigo hicho, lakini akitetea vijana wake kuwa, mvua ndio chanzo cha kushindwa kuhimili vishindo vya watetezi hao.
“Mvua imekuwa ikitukwamisha kiukweli maana nashindwa kabisa kupata muda wa kuendelea na programu zangu, hasa baada ya kugundua kupitia michuano ya Kombe la Muungano," alisema Mkalambati.
Katika mchezo mwingine kwa timu za wanawake, Magereza iliikimbiza Jeshi Stars kwa kuinyuka seti 3-2 na kuwafanya washindi hao kuongoza msimamo ikiwa na pointi nane, huku wapinzani wao wkiwafuata nyuma yao na alama zao sita.
Nahodha wa Jeshi stars, Doreen Kobelo, alisema licha ya kipigio lakini bado anaamini timu yao ina nafasi ya kubeba taji la michuano hiyo msimu huu.
Previous
Next Post »