JPM: ATAKAYEJARIBU KUVUNJA MUUNGANO, ATAVUNJIKA YEYE - Rhevan Media

JPM: ATAKAYEJARIBU KUVUNJA MUUNGANO, ATAVUNJIKA YEYE

Tokeo la picha la MUUNGANO DODOMA

Rais Dk. John Magufuli, akikagua gwaride la heshima wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana.
RAIS Dk. John Magufuli ameonya kuwa mtu yeyote atakayejaribu kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar atavunjika yeye.
Aliyasema hayo jana mjini hapa, alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Jamhuri kuadhimisha miaka 53 ya Muungano huo.
Maadhimisho hayo ni ya kwanza kufanyika mkoani Dodoma tangu kuundwa kwa Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar.
 “Katika kutunza Muungano wetu, taifa la Tanzania litasonga mbele, kama nilivyoahidi mimi na Dk. Shein (Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein). Leo tunasherehekea miaka 53 wakati tunatambua kabisa wenzetu waliotutangulia waliutunza Muungano huu kwa nguvu zote, wakina mzee Mwinyi (Ali Hassan), akina mzee Mkapa (Benjamin) akina mzee Jumbe (Aboud Jumbe), mzee Mkapa usilalamike wewe ni mzee sasa hivi, akina mzee Kikwete (Jakaya) pamoja na kwamba yeye anaonekana ni kijana kuliko mimi, ni kwa sababu ya shida tu.
“Unajua kuongoza nazo ni shida sana, siku hizi amekuwa kijana zaidi (Kikwete) anapendeza, napenda kurudi kuwaahidi ndugu zangu Watanzania, Muungano ndiyo silaha yetu, Muungano ndiyo jembe letu, Muungano ndiyo umoja wetu, Muungano ndiyo ushindi wetu, nataka niwahakikishie, mimi pamoja na Dk. Shein, tutaulinda Muungano kwa nguvu zote na kamwe asijitokeze mtu yeyote atakayejitahidi au kujaribu kuuvunja Muungano, atavunjika yeye,” alisema Rais Magufuli.
Pia alizungumzia umuhimu wa amani kuwa ni jambo la msingi na la kulinda kwa nguvu, kwa sababu ndiyo iliyofanya leo Muungano wa Tanzania na Zanzibar ukafikisha miaka 53.
“Waimbaji wameimba, tunaweza kufikisha miaka 53 ya Muungano kwa sababu ya amani na tunaweza kupata mafanikio yote tuliyonayo kwa sababu ya uwepo wa amani, hapa nchini bila ya amani mambo yote haya yasingewezekana,” alisema Rais Magufuli.
KUHAMIA DODOMA
Kuhusu ahadi yake ya Serikali yote kuhamia Dodoma ifikapo 2020, alisema hadi sasa zaidi ya watumishi 3,000 wameshahamia Dodoma.
Alisema pia katika bajeti inayoendelea kujadiliwa na Bunge sasa hivi, takribani Sh bilioni 200 zimetengwa kwa ujenzi wa ofisi za Serikali na nyumba za viongozi.
Dk. Magufuli alisema katika kuhakikisha Dodoma inapata hadhi ya kuwa Makao Makuu ya nchi, uwanja wa ndege wa Dodoma umetanuliwa, jiwe la msingi la reli ya kisasa ambayo pia itapita Dodoma limewekwa na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine unaendelea.
Alitaja maandalizi mengine yanayoendelea kuwa ni pamoja na kuhakikisha umeme wa uhakika na maji vinapatikana na pia kuhakikisha kuna huduma za afya na elimu.
MAKOMANDOO
Maonyesho ya makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na yale ya kikundi cha chipukizi kinachoundwa na wanafunzi wa shule za sekondari za Dodoma, ambao Dk. Magufuli aliwaita ‘makomandoo watarajiwa’, yamefanya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano kuwa ya aina yake.
Baada ya gwaride la kawaida linaloundwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kumalizika, lilifuata onyesho la ukakamavu lililofanywa na makomando wa JWTZ, lililowaduwaza viongozi waliohudhuria maadhimisho hayo.
Baadhi ya maonyesho hayo ni pamoja namna ya kucheza karate, kumshambulia adui, kuvunjiwa tofali kichwani, kubeba wenzao kwa meno, kukunja nondo na kupigwa na mbao sehemu mbalimbali za mwili bila kudhurika.
Rais Mstaafu, mzee Ali Hassan Mwinyi, alionekana kutingisha kichwa wakati mmoja wa makomando alivyompiga kichwani mwenzake wakati wakifanya onyesho hilo.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, naye alionekana kuduwaa muda mwingi wakati kikosi hicho kilipokuwa kikifanya matukio, huku akionekana akizungumza jambo na Mkuu wa Jeshi hilo, Jenerali Venance Mabeyo.
Wakati wakifanya hivyo kwa kupokezana, mshereheshaji alisema makomandoo hao ni wale walioshiriki katika mapigano ya M23 katika nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
GWARIDE LA WANAFUNZI
Gwaride la wanafunzi wa sekondari za mjini Dodoma  lilijumuisha wasichana na wavulana likiwa na vikosi vinne, huku vitatu vikiwa ni vya askari wa kawaida na kimoja cha makomandoo.
Vikosi hivyo, vilikuwa na viongozi wake kama vilivyo vile vya majeshi ya ulinzi na usalama na vilingia uwanjani na kutoa heshima kwa Rais kabla ya kusimama katikati ya uwanja na kuimba wimbo wa ‘Tazama Ramani’.
GWARIDE LA MBWA
Kulikuwa na gwaride la mbwa ambao walikuwa wakifanya kila wanachoelekezwa na askari wao.
Mbali na hilo, pia kulikuwa na mbwa wa kufichua bangi. Mmoja wa askari alificha bangi na baadaye mbwa akaitafuta kwa kunusa hadi alipoipata.
Mbwa mwingine aliyeonyesha umahiri ni wa kufichua wahalifu. Watu wawili waliigiza kama wahalifu na baadaye kushambuliwa kwa kung’atwa na mbwa hao.
JK KIVUTIO
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, aliwasili saa 2:20 asubuhi Uwanja wa Jamhuri na baada ya kutambulishwa na mshereheshaji, uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe. 
Previous
Next Post »