Dodoma. Rais John Magufuli ameahidi kuulinda kwa nguvu zote na yeyote anayetaka muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjike, atavunjika yeye.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika hotuba yake ya dakika 20 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma yalikofanyika maadhimisho hayo kwa mara ya kwanza tangu Serikali ihamie mjini hapa.
“Mimi na Dk (Ali Mohamed) Shein tutaulinda kwa nguvu zote, kamwe asijitokeze mtu yeyote atakayejitahidi au atakayetaka kuuvunja Muungano huu. Atakayefanya hivyo atavunjika mwenyewe,” alisema Rais Magufuli akihitimisha hotuba yake.
Vilevile, Rais Magufuli alisema, “Muungano ndiyo silaha yetu, Muungano ndiyo jembe letu, lazima tuudumishe.”
Hata hivyo, alisema ingawa kitu kinachoitwa muungano ni kigumu kama ndoa ilivyo ngumu kuidumisha, wapo watu ambao kwa miaka 53 walifanya kazi usiku na mchana kuudumisha hadi kufikia hapo.
Aliwataja baadhi ya walioshiriki kuudumisha Muungano huo kuwa ni waasisi Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Wengine kuwa ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete. Mkapa hakuwepo kwenye sherehe hizo.
Habari Zinazohusiana
Sign up here with your email