TFF HALI SI SHWARI - Rhevan Media

TFF HALI SI SHWARI



Rais wa TFF,Jamal Malinzi
Rais wa TFF,Jamal Malinzi 

Dar es Salaam. Hali si shwari ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumebainika kuwa mgogoro baina ya watendaji wa shirikisho hilo.
Habari za ndani zinaeleza, rais wa TFF, Jamal Malinzi amewekwa kiti moto baada ya kudaiwa kuwabadilisha watia saini wa benki huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikianza kuwahoji baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo.
Ingawa Takukuru haikuwa tayari kulizungumzia suala hilo, lakini habari zaidi zinasema viongozi kadhaa wa TFF wamehojiwa na Taasisi hiyo wakihusishwa na matumizi mabaya ya fedha za shirikisho hilo.
Mbali na Takukuru, pia imeelezwa kuwepo kwa maelewano mabaya baina ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ya TFF huku kikao cha Machi 26 kikipangwa kutumika kumuhoji Malinzi juu ya madai ya kughushi muhtasari na kubadili watia saini.
Baadhi ya wajumbe katika kikao hicho wameeleza kutojua ajenda ingawa tayari wamepokea barua za wito wa kikao.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas ilisema jana kuwa kikao kitafanyika Dar es Salaam na ajenda kuu itakuwa kupanga tarehe ya uchaguzi mkuu wa shirikisho utakaofanyika baadaye Oktoba.
“Wataanza kufungua kikao, kisha mengineyo na baadaye kufunga kikao, masuala mengine yanayosemwa ni siasa hakuna chochote,” alisema Lucas.
Makamu wa rais wa TFF, Walence Karia alikiri kupewa taarifa za kikao, lakini akasisitiza masuala mengine aulizwe katibu mkuu, Celestine Mwesigwa.
“Habari za kughushi muhtasari na kubadili watia saini wa benki mimi siwezi kulizungumzia, hilo ni suala la Katibu Mkuu kwanza silifahamu,” alisema Karia kwa kifupi.
Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alipotafuwa alisema yuko na majukumu mengine hawezi kuzungumza chochote.
Previous
Next Post »