Dar es Salaam. Wakati mashirika na kampuni binafsi zikifanya vizuri, mashirika na taasisi za Serikali zimejikuta zikishindwa kutoa huduma au kukabiliana na ushindani kutokana na sababu tofauti, kuu ikiwa ni madeni zinazodai wadau wake.
Na mdau mkuu anayedaiwa ni Serikali, ambayo imekuwa ikichelewesha malipo ya huduma inazopewa na mashirika na taasisi hizo kiasi cha baadhi kutetereka, kudhoofika na mengine kutishia uhai wake.
Si Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Hifadhi ya Jamii (NSSF), mamlaka za maji za mikoa, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wala Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF). Yote yana kilio kimoja; deni kubwa la Serikali.
Rais John Magufuli anaweza kuwa ameanza kutafuta suluhisho la udhaifu wa mashirika na taasisi hizo baada ya kuanza kutoa amri za kuwataka viongozi wanaoongoza taasisi hizo kuhakikisha wanafuatilia madeni bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Alianza kwa kuiamuru NHC kuwaondoa wateja wasiolipa fedha za pango bila ya kujali itikadi na hivi karibuni aliiagiza Tanesco pia kuchukua uamuzi kama huo, akiitaka ithubutu kuikatia umeme hadi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayodaiwa Sh121 bilioni.
Hayo ni maagizo kwa taasisi mbili, bado kuna orodha ndefu ya mashirika ambayo yanafanya vibaya kutokana na kushindwa kukusanya ipasavyo malipo ya huduma zake kutokana na ukweli kuwa mteja mkuu ni Serikali.
Hatua hiyo itaweza kuimarisha mashirika hayo endapo itakuwa endelevu kutokana na mengi kulalamikia ucheleweshwaji wa muda mrefu wa malipo.
Oktoba 28 mwaka jana, aliyekuwa mkururugenzi mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba aliieleza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba shirika hilo linaidai Serikali jumla ya Sh125 bilioni kutokana na huduma inazotoa kwa mashirika ya umma na Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco).
Ukiacha mikataba mibovu na kashfa ambazo zimekuwa zikilikumba shirika hilo, madeni hayo makubwa yamechangia Tanesco kushindwa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.
Rais Magufuli ameitaka Tanesco kuchukua hatua za kijasiri kukusanya madeni hayo.
Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ilibainisha NSSF ilikuwa inadai Sh723 bilioni ambazo Serikali ilikopa kwa ajili ya miradi mbalimbali. Kuchelewa kwa malipo hayo kulilifanya deni hilo kukua hadi kufikia Sh729.2 bilioni kutokana na riba.
Pia, MSD imekuwa ikishindwa kuhudumia hospitali za umma kwa kuzisambazia dawa na vifaa tiba kutokana na Serikali kutolipa kwa wakati madeni yake ambayo wakati fulani yalifikia Sh90 bilioni.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ilikuwa kati ya waathirika wa huduma za MSD baada ya kushindwa kulipa Sh8 bilioni. Ilifikia wakati mashine za vipimo za MRI na CT Scan zilishindwa kufanya kazi kwa wiki kadhaa kutokana na hospitali hiyo kushindwa kuzitengeneza.
Shirika lililoathirika zaidi na madeni hayo kiasi cha kulalamikiwa huduma zake ni PSPF ambayo deni lake lilifikia Sh7.9 trilioni kati ya Sh8.43 trilioni ambazo mifuko ya hifadhi ilikuwa ikiidai Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ya mwaka jana, PSPF inaweza kuimarika na uhai wake kudumu hadi mwaka 2075 iwapo italipwa michango ya kabla ya mwaka 1999 mafao yatarekebishwa au michango kuongezwa hadi kufika asilimia 28 badala ya asilimia 20.
Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi.
Sign up here with your email