DK MAHANGA MATATANI TENA MAHAKAMA YAAMURU AKAMATWE - Rhevan Media

DK MAHANGA MATATANI TENA MAHAKAMA YAAMURU AKAMATWE

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga ameingia matatani tena baada ya Mahakama Kuu kuamuru akamatwe na kufikishwa mahakamani hapo.
Amri hiyo ilitolewa na Naibu Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu, Ruth Masambu wiki iliyopita baada ya Dk Mahanga kushindwa kufika mahakamani hapo bila taarifa.
Dk Mahanga ambaye alikuwa mbunge wa Ukonga na baadaye Segerea kwa tiketi ya CCM, alitakiwa kufika mahakamani hapo Alhamisi iliyopita ili kulipa Sh2 milioni, ikiwa ni sehemu ya deni la zaidi ya Sh11 milioni anazodaiwa.
Mwanasiasa huyo ambaye sasa ni kada wa Chadema, anadaiwa kiasi hicho na mwanaharakati wa haki za binadamu, Kainerugaba Msemakweli ikiwa ni gharama alizozitumia katika kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa dhidi yake na Dk Mahanga.
Dk Mahanga alifungua kesi ya madai namba 145 ya mwaka 2009 akidai kuwa kitabu alichoandika mwanaharakati huyo cha “Orodha ya Mafisadi wa Elimu Tanzania” kikimtaja kuwa ni mmoja wa vigogo wenye shahada za udaktari wa falsafa za kughushi, kilimdhalilisha.
Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa Julai Mosi, 2014 kutokana na Mahanga na mawakili wake kutofika mahakamani mara kwa mara.
Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi










Previous
Next Post »