Maafisa Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutumia tovuti za ofisi na tovuti kuu ya Serikali kwa kuweka taarifa mbalimbali zinazohusu huduma na bidhaa zinazotolewa na taasisi hizo ili kuwawezesha wananchi kuzifahamu huduma hizo kirahisi.
Rai hiyo imetolewa leo Mkoani Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (EGA), Dkt. Jabir Bakari alipokuwa akitoa semina juu ya matumizi na umuhimu wa tovuti za Serikali katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano Serikalini kinachoendelea Mkoani humo.
Dkt. Bakari amesema dhana ya Serikali Mtandao ni kuhuisha matumizi ya TEHAMA kwenye utoaji wa taarifa mbalimbali za Serikali kwa wananchi hivyo ni muhimu kwa kila taasisi kuwa na tovuti zenye taarifa za uhakika na zinazoendana na wakati ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
“Wakala kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo tumetengeneza mfumo unaotumia muda mfupi kwa taasisi za Serikali kutengeneza tovuti zao ili ifikapo Juni mwaka huu taasisi zote ziwe na tovuti zao zitakazowarahisisha wananchi kufahamu huduma kirahisi,”alisema Dkt.Bakari.
Mtendaji Mkuu huyo ameongeza kuwa tovuti za taasisi zisitumike tu katika kutoa taarifa za huduma na bidhaa zao bali zitumike kuelezea mambo mengine muhimu yanayofanywa na taasisi hizo.
Akielezea kuhusu tovuti kuu ya Serikali, Dkt. Bakari amesema ni muhimu kuhakikisha taarifa muhimu na za kudumu za taasisi husika zinawekwa ili kusaidia wananchi kufahamu kiundani kazi wanazozifanya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano (TAGCO), Bw.Innocent Mungy amesema mbali na kuweka taarifa katika tovuti za Serikali, ni wajibu wa Maafisa Mawasiliano Serikalini kutumia mitandao ya kijamii kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi .
“Kutokana na maendeleo ya teknolojia duniani hasa katika upande wa mawasiliano, matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakileta tija kwa taasisi za Umma kwani yanasaidia Serikali kujibu haraka hoja zinazowasumbua wananchi”alisema Mungy.
Pia aliwataka Maafisa Mawasiliano kuwa wabunifu katika kutumia mitandao ya kijamii kwani mitandao hiyo inatoa fursa ya kushirikiana, kutangaza huduma na bidhaa za taasisi, kufahamu matatizo ya wananchi.
Sign up here with your email