Polisi mkoani Ruvuma inamshikilia Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kitanda wilayani Namtumbo, Gislary Tweve kwa tuhuma za kumshambulia mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kitanda, Adolf Nyoni (34) baada ya kukataa kulipa kinywaji aina ya Konyagi, kilichokuwa katika kifungashio cha plastiki (kiroba) alichokunywa katika duka la kanisa hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zuberi Mwombeji alisema padri huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 10, mwaka huu, saa mbili usiku katika duka la Parokia ya Kitanda.
Kamanda Mwombeji alisema Padri Tweve alimpiga Nyoni kichwa na makofi, kisha kumrukisha kichura kwa kile kinachodaiwa kukataa kulipa pombe hiyo ambayo imekatazwa kisheria, lakini duka hilo bado limekaidi na kuendelea kuuza pombe hiyo.
Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na mara utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma, kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali katika vyombo vya dola, badala ya kujichukulia sheria mkononi na kuachana na biashara iliyopigwa marufuku ya pombe kali zilizofungwa kwenye vifungashio vya plastiki.
Kuanzia Machi mosi, mwaka huu, serikali imepiga marufuku utengenezaji, usambazaji, uuzaji na unywaji wa pombe zilizowekwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kwa jina la viroba, na kuibainisha kuwa itatoa adhabu zikiwemo faini za hadi Sh milioni tano, kifungo jela au vyote kwa pamoja, kwa watakaokiuka marufuku hiyo.
Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubainika kwamba mbali ya kuikosesha mapato serikali yanayofikia Sh bilioni 600 kwa mwaka, pombe hizo za kwenye viroba zimekuwa zikitumiwa isivyo kutokana na ufungashaji wake wa kirahisi.
Sign up here with your email