DALALI AIPA MBINU SIMBA YA KUIPORA UBINGWA YANGA - Rhevan Media

DALALI AIPA MBINU SIMBA YA KUIPORA UBINGWA YANGA

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Sc, Hassan Dalali ameipa siri klabu hiyo ya kuvunja mwiko wa kutochukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa misimu minne mfululizo, ambapo mara ya mwisho ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2011/12.
Dalali amesema kilichosababisha klabu hiyo kuporwa ubingwa na watani wao wa jadi Yanga Sc msimu wa 2012/13 , ni uongozi na wanachama wa timu hiyo kukosa ushirikiano tangu ulipomalizika uchaguzi wa kuchagua viongozi wa klabu hiyo, pamoja na baadhi ya viongozi wake kuifanya klabu kama kitega uchumi.
Amesema ili Simba SC ichukue ubingwa wa VPL msimu wa 2016/2017 lazima wanachama wake wawe na umoja huku akiutaka uongozi wa klabu hiyo kuwasamehe sambamba na kuwarudishia uanachama wanachama wake 72 waliofukuzwa uanachama kutokana na kuishitaki klabu hiyo mahakamani.
“Kama tunataka ushindi inabidi tushikamane, wale walioitwa Simba Ukawa warudishIwe uanachama ili kuondoa matabaka kama mimi nilivyowasamehe wanachama zaidi ya 600 pamoja na Evance Aveva ambaye kwa sasa ni Rais wa timu. Baada ya kuwasamehe timu ilikuwa na umoja na mshikamano na tulifanya vizuri tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna matabaka kuanzia kwenye uongozi hadi kwa wanachama,” amesema.
Previous
Next Post »