SHULE ZA BINAFSI ZAZIDI KUTIKISA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE - Rhevan Media

SHULE ZA BINAFSI ZAZIDI KUTIKISA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa, Dk Charles Msonde akitangaza matokeo ya mtihani ya kidato cha nne wa mwaka 2016, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis 

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2016 yakionyesha Mkoa wa Dar es Salaam umetoa shule sita kati ya 10 zilizofanya vibaya kitaifa, huku Feza Boys ya mkoa huo ikiongoza kwa ufaulu kitaifa.
Hata hivyo, katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, mkoa huo umetoa shule tatu katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.
Kadhalika, shule za Serikali zimeendelea kuadimika katika orodha ya 10 bora kitaifa kwa mwaka wa tano mfululizo.
Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2011 wakati shule za Mzumbe ya Morogoro na Kibaha ya Pwani ziliposhika nafasi ya tisa na 10 mtawalia.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.56 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Mwaka 2015 kiwango cha ufaulu kilikuwa ni asilimia 67.53 wakati mwaka 2016 kimepanda hadi asilimia 70.09.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa 349,524 waliofanya mtihani huo, waliofaulu ni 244,762 sawa na asilimia 70.35.
Kati yao, wasichana waliofaulu ni 119,896 sawa na asilimia 67.34 wakati wavulana ni 124,866 sawa na asilimia 73.50.
“Kulingana na takwimu hizi, ufaulu wa jumla wa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia 2.44 ikilinganishwa na mwaka 2015,” alisema Dk Msonde.
Alisema watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 32,521 sawa na asilimia 68.19 wakati mwaka 2015 waliofaulu ni 31,951 sawa na asilimia 64.80.
Dk Msonde alisema watahiniwa wa shule waliopata daraja la kwanza ni asilimia 2.76, daraja la pili asilimia 9.31, la tatu asilimia 15.57, la nne asilimia 42.75 walioshindwa asilimia 29.65.
Kuhusu ufaulu katika masomo, Dk Msonde alisema Hisabati ndiyo imekuwa ngumu kwa wengi ikiwa na ufaulu wa asilimia 18.12 wakati somo lenye ufaulu wa juu ni Kiswahili lenye asilimia 77.75.
“Kwa ujumla, ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya Hisabati, Jiografia, Kiswahili, Biashara na Book-Keeping na Lugha ya Kiingereza umepanda kwa kati ya asilimia 0.12 na 8.08 ikilinganishwa na mwaka 2015,” alisema.
Kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora, aliyeibuka kinara ni Alfred Shauri wa Feza Boys (Dar es Salaam) akifuatiwa na Cyntia Mchechu kutoka St Francis (Mbeya).
Waliofuata ni Jigna Chavda (Marian Boys – Pwani), Naomi Tundui (St Mary Goreti (Kilimanjaro), Victoria Chang’a (St Francis –Mbeya), Brian Johnson (Marian Boys – Pwani), Esther Mndeme (St Mary’s Mazinde Juu –Tanga), Ally Koti (ALCP Kilasara – Kilimanjaro) na Emmanuel Kajege (Marian Boys – Pwani ).
Feza Boys ya Dar es Salaam iliibuka kinara kitaifa ikifuatiwa na St Francis Girls (Mbeya), Kaizirege (Kagera), Marian Girls na Marian Boys, St Aloysius Girls (Pwani), Shamsiye Boys (Dar es Salaam), Anwarite Girls (Kilimanjaro), Kifungilo Girls (Tanga) na Thomas More Machrina (Dar es Salaam).
Mbali hizo, Dk Msonde alizitaja shule kumi zilizofanya vibaya kitaifa kuwa ni Kitonga na Nyeburu za (Dar es Salaam), Masaki (Pwani), Mbopo, Mkondole na Somangila Day (Dar es Salaam), Dahani (Kilimanjaro), Ruponda (Lindi), Makiba (Arusha) na Kidete (Dar es Salaam).
Dk Msonde alisema Necta imezuia matokeo ya watahiniwa kutoka shule 33 ambao walipata matatizo mbalimbali ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa sababu hizo za ugonjwa,” alisema.

Previous
Next Post »