MBOWE AWAITA MAMEYA WA DAR KUJADILI UUZWAJI WA UDA - Rhevan Media

MBOWE AWAITA MAMEYA WA DAR KUJADILI UUZWAJI WA UDA

Tokeo la picha la MAGARI YA UDA
HISA za Uda zawa kaa la moto. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kufanya kikao cha dharura na mameya, naibu mameya na viongozi waandamizi wa Ukawa kujadili utata wa uuzwaji wa hisa za Shirika hilo la Usafiri Dar es Salaam.

Mameya hao kutoka Dar es Salaam waliwasili mjini hapa juzi kwa nyakati tofauti, kuhudhuria kikao hicho kilichofanyika jana kwenye ofisi za Bunge.

Taarifa zilizotufikia zilieleza kuwa kikao hicho kilifanyika baada ya kuibuka mvutano kati ya Serikali na uongozi wa Jiji hilo, linaloongozwa na Ukawa kuhusu kuidhinisha Sh bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa kampuni ya Simon Group.

Jumamosi iliyopita Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo chini ya Meya wake, Isaya Mwita kwenye kikao chake cha kawaida, lilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kilichoelezwa ni sawa na kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi kidogo.

Kikao hicho kilifanyika baada ya agizo la Rais John Magufuli Januari 27 wakati akizindua mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Katika agizo hilo, Rais alitoa siku tano kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha kiasi hicho cha fedha zilizolipwa na Simon Group kinapangiwa matumizi.

Lakini jana, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema alisema nje ya viwanja vya Bunge, kuwa amewaita mameya hao na manaibu wao ili kuzungumzia sakata la hisa hizo.

“Nataka tupate msimamo wa pamoja ili wakazi wa Dar es Salaam wanufaike na na Uda. Sioni sababu ya kuiua wala kulichukia shirika hili,” alisema.

Miongoni mwa mameya walioonekana jana kwenye viwanja vya Bunge ni Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye alikiri kuitwa kuhudhuria kikao licha ya kusisitiza kuwa hajui ajenda.

Mapema jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hana la kusema juu ya kushindwa kugawanywa kwa fedha hizo.

Alitaka viongozi hao wapewe muda ili kumaliza tatizo hilo huku akisisitiza kwamba kwa kuwa siku zimepita, anasubiri kauli ya Rais juu ya jambo hilo.
Previous
Next Post »