Mwenyekiti wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni (katikati) akiwa ameshikana mikono na viongozi wa kamati ya utendaji wa Simba, Rais wa Klabu ya Simba Evance Aveva, Mkuu wa kitengo wa habari na mawasiliano Haji Manara, Mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hanspope.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Simba limekubali yaishe baada ya kukutana leo na na Kamati ya utendaji ya Klabu hiyo na kuwataka wapeleke mpango kazi wa mabadiliko ili kufikia maamuzi yatakayokuwa na manufaa ndani ya klabu hiyo kongwe hapa nchini.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mzee Hamis Kilomoni alisema wanatambua kila binadamu anafanya makosa na kama mtu akifanya kosa hakuna budi kumsamehe na kushirikiana kufanya mambo mbalimbali ambayo yataleta maendeleo.
Alisema Kamati hiyo ilifanya vikao vyake na kugundua Uongozi wa Simba kwa ujumla ulikosea kufanya maamuzi yake na kuamua kuwasamehe kwa yote waliyoyakosea ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo kutoka kumilikiwa na wanachama na kuelekea kwa mwekezaji mmoja. Ikumbukwe kuwa baraza hilo liligomea hatua za mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo yaliyotangazwa kufanywa na kamati tendaji tangu mwaka jana kwa madai ya kutotimiza matakwa mbalimbali ya kisheria ikiwemo kupuuzia baraza hilo linalotambulika kisheria.
"Niwajulishe mashabiki wa Simba kwa ujumla kwamba sisi hatuna ugomvi na Kamati tendaji ya Simba lakini kilichokuwa kikifanyika ni kuwashtua watekeleze matakwa yale tuliyokuwa tukiwaeleza kwa muda mrefu na wao walikuwa hawajayatekeleza kikubwa zaidi hakuna mtu anayekataa mabadiliko na sisi kama bodi ya wadhamini ya Simba SC ambao tunapenda kuona mafanikio ya klabu tumewaagiza hawa viongozi watuletee mpango kazi ili tujue ni namna gani mabadiliko hayo yatakavyokuwa na msaada kwa klabu kiujumla," alisema Kilomoni.
Kilomoni aliendelea kusisitiza kuwa licha ya kuwataka viongozi wa klabu hiyo kupeleka mpango kazi ili wafanye mabadiliko, Viongozi hao wanapaswa kutambua mali zilizopo katika klabu hiyo ni za Simba hazitokwenda kwa yeyote badala yake zitaendelea kubaki chini ya baraza la wadhamini kama ilivyokuwa kipindi chote na mali za klabu hiyo sio za mchezo wa mpira wa miguu pekee bali zinauhusiano na michezo mingine licha ya kuwa kwa sasa haipo katika klabu hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva alisema kumekuwa na taarifa za kutokuwepo kwa maelewano chanya kati ya Uongozi wa klabu hiyo na baraza la wadhamini jambo ambalo limemsukuma na kujitokeza kulizungumzia ili kuwajuza watanzania kwamba hakuna tatizo lolote.
Alisema kilichokuwa kikitokea katika klabu hiyo ni changamoto za kufanya kazi kwa pamoja na sehemu zote zinazowakutanisha watu mbalimbali kutokea kwa baadhi ya watu kukubali jambo fulani na wengine kutokubali ni lakawaida na halishangazi sana kwa kuwa Simba sio ya kwanza kupitia hilo.
Alisema uongozi wa Simba umekuwa ukifanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka zote zilizopo katika klabu hiyo ili kuhakikisha inapata mafanikio yale waliyoyapata kwa wakati waliojipangia na kuahidi kufanyia kazi kwa wakati maelezo yaliyotolewa na baraza la wadhamini.
Rais wa Klabu ya Simba Evance Aveva akizungumza na waandishi wa habari juu ya mustakabali wa uhalali wa Simba na bodi ya wadhamini na kukubaliana kuweka wazi michakato yote ya mabadiliko ya klabu hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni.
Mwenyekiti wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni akizungumza na waandishi wa habari juu ya mustakabali wa uhalali wa Simba na bodi ya wadhamini na kukubaliana kuweka wazi michakato yote ya mabadiliko ya klabu hiyo.
Sign up here with your email