YOWE LA WENYE NYUMBA LAMTOA ROHO BAADA YA KUIBA KUKU MMOJA - Rhevan Media

YOWE LA WENYE NYUMBA LAMTOA ROHO BAADA YA KUIBA KUKU MMOJA

Tokeo la picha la DIRISHA LA NYUMBA

Mwanza. Mkazi wa Kijiji cha Kanyerere, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Safari Bungate (51) ameuawa baada ya kushambuliwa na kundi la watu kutokana na kutuhumiwa kuiba kuku wa mwenye nyumba wake, Matetema Mathias (40).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea Januari 26, saa nne usiku baada ya mwenye nyumba huyo kumsikia mtuhumiwa akiingia ndani kupitia dirishani na kuiba kuku mmoja.
“Wakati anaondoka, mwenye nyumba alimuona na kupiga mayowe kuomba msaada,” alisema Msangi.
Alisema baada ya majirani kuamka walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na kuku, walianza kumshambulia kwa mawe hadi kupoteza fahamu baada ya muda mfupi alifariki dunia.
Msangi alisema wanamshikilia Mathias kwa mahojiano zaidi.
Katika hatua nyingine, polisi wamekamata pikipiki 217 na bajaji 27 ambazo zilikutwa na makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Kamanda Msangi alisema operesheni hiyo ambayo ilianza hivi karibuni, imewakumba abiria 31 wa pikipiki ambao walikutwa bila kuvaa kofia ngumu.
Msangi alisema miongoni mwa makossa yaliyosababishwa na pikipiki hizo ni waendeshaji kutofuata sheria za barabani, kutokuwa na leseni, kutovaa kofia ngumu, kubeba zaidi ya abiria mmoja, kuvunja namba za usajiri na kuendesha wakiwa wamelewa.
Makosa mengine ni kuongeza ukubwa wa mafla, kitendo ambacho ni kinyume na sheria. Alisema operesheni hiyo imetokana na uwapo wa matukio mengi ya ajali za barabarani zilizosababisha watu kupoteza maisha na ulemavu wa kudumu.
“Polisi tumeanza kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, kufanya vikao na vikundi vya waendesha pikipiki na elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi,” alisema.







Previous
Next Post »