MWANASIASA mkongwe na waziri katika serikali ya awamu ya tatu, Ali Ameir Mohamed, ameibua hoja nzito kuhusu urais wa Zanzibar huku akipinga suala la uongozi wa kurithishana.
Katika hoja hiyo ambayo imekuja wakati kukiwa na madai ya baadhi ya Wazanzibari wenye historia kuanza kampeni za chini chini kwa ajili ya kugombea Urais 2020, Ameir amesema si busara kumpata kiongozi wa ngazi yoyote ya kisiasa au serikali kwa kigezo kwamba baba, babu au bibi yake alikuwa ama Rais, Mwakilishi, Mbunge au Mtendaji wa chama.
Badala yake, Ameir ametaka kiongozi apatikane kutokana na uchapakazi, uzalendo, ufahamu, uhusiano na uwezo binafsi.
“Wakati wa kumtafuta na kumpata kiongozi kwa sababu ya Ukaskazini, Ukusini, Upemba, Uunguja au Uumjini wake, umepita na usikubalike tena kama kigezo cha msingi chenye umuhimu na maana kabla ya kiongozi mhusika hajakabidhiwa dhamana ya uongozi,” alisema Ameir ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Habari na Siasa).
Akizungumza jana nyumbani kwake Donge, mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema kwa miaka mingi wakati Zanzibar ikitawaliwa kisultani, kiongozi hakupatikana kwa sifa, uwezo wake, elimu au uaminifu wake bali kwa sababu tu alitoka katika ukoo wa kifalme.
"Kwa muda mrefu baadhi ya watu hususan baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, ilijengeka nadharia kuwa Rais lazima apatikane kwa asili ya maeneo. Zama hizo zimekwisha, amepatikana toka Mjini, Kusini, Kaskazini na Pemba, sasa sifa, uwezo binafsi, uchapakazi, uzalendo, upeo na ujasiri ziwe ndizo sifa za msingi," alisema.
Pia alisema serikali za vyama vya TANU na ASP, baada ya Uhuru na Mapinduzi, zilipiga marufuku tawala za kichifu, kisultan na kimwinyi hatimaye ikafunguliwa milango ya demokrasia, kuundwa kwa katiba kwa mujibu wa sheria bila kutazama nasaba, rangi, kabila au imani ya dini.
Kwa mantiki hiyo, alisema haipaswi mtu kupewa madaraka yoyote kwa kigezo cha baba, bibi au babu yake aliwahi kushika wadhifa fulani na haitakuwa haki akanyimwa mtu anayeonekana anatosha kivigezo kwa sababu huko nyuma mtu mmoja katika familia yake alishika wadhifa fulani.
"Kusudio la kuundwa katiba za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na (ya) Zanzibar hatimaye kuwepo kwa sheria zake ni kutoa haki katika muktadha wa usawa, demokrasia na wajibu. Azma yoyote au ishara ya kurudisha usultani au uchifu ipingwe bila muhali.”
Ameir alisema kiongozi anayepatikana kwa sababu ama ya ukabila, udini, asili au nasaba hawezi kuwa na nafasi au kutazama maslahi mapana kulingana na matakwa ya dunia ya sasa wala vyeo au madaraka ya kisiasa na utawala yasitegemee nguvu za fedha, urithi au nasaba kwani mnaweza kujikuta mkirudi mahali mlikokukataa.
Pia mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuendeleza ukabila, asili au mgombea wa ngazi yoyote aungwe mkono kwa minajili ya misukumo hiyo, alionya akisema hiyo si msingi iliyowekwa na waasisi wa taifa kwa mustakabali wa kukuza dhana ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na demokrasia.
"Alipatikana Rais Julius Nyerere kwa sifa, uwezo na uzalendo wake, akaja Mzee Ali Hassan Mwinyi, akafuata Benjamin Mkapa, baadaye Dk. Jakaya Kikwete na sasa yupo Rais Dk. John Magufuli kwa msingi ile ile iliyowekwa ambayo imelipatia heshima ya juu taifa letu,” alisisitiza.
MACHO MAKINI
Dhamana ya uongozi wa juu, kwa mujibu wa Ameir, inahitaji kwanza mtu apimwe na wenzake wanaomtazama kwa macho makini na utayari wake badala yeye mwenyewe au wapambe wake kuanza kupitapita na kumpiga debe mitaani wakimsemea anatosha au anafaa.
Ameir alisema heshima inayopewa Tanzania na mataifa mbalimbali duniani ni kutokana na uongozi wake wa juu unavyoweza kuchemsha bongo, kutafakari kwa kina au kupitisha uamuzi na kuthubutu kusema fulani amekiuka taratibu na maadili, hivyo hastahili hatimaye akaondolewa bila kuutazama uso au rangi yake.
"Uamuzi au hatima yenye kubeba dhamana ya maisha na uhai wa binadamu unahitaji sana tahadhari na umakini, mkiendesha mambo ambayo nyeti kienyeji na kwa urahisi huku mkitazamana usoni na kuoneana aibu, hamtafika mbali," alionya mwanasiasa huyo nguli. "Mtajikuta siku moja mnaharibikiwa."
Mtazamo wa mwanasiasa huyo mkongwe Zanzibar umekuja siku chache tangu Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuonya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojinadi chinichini kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kuacha kufanya hivyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar na televisheni ya Azam, Rais Shein alisema wanaotamani urais wajue muda bado.
Sign up here with your email