SILAHA ZA KIVITA, NYARA ZA SERIKALI ZA SH MILIONI 131 ZAKAMATWA TABORA - Rhevan Media

SILAHA ZA KIVITA, NYARA ZA SERIKALI ZA SH MILIONI 131 ZAKAMATWA TABORA

Picha inayohusiana
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameshuhudia aina mbalimbali za silaha, zikiwamo za kivita 61 na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh milioni 131 zilizokamatwa hivi karibuni mkoani Tabora.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa silaha na nyara hizo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Seleman, alisema silaha hizo zilikamatwa kutokana na operesheni maalumu iliyofanywa na polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Idara ya Maliasili mkoani hapa.
Alisema operesheni hiyo, ililenga kupambana na majangili na wafanyabiashara haramu wa nyara  za Serikali, baada ya kupata taarifa za kiintelijensia zilizofanywa kistaarabu pasipo kutumia nguvu kubwa.
“Silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni SMG 12, Rifle 6, Shotgun 2, magobole 41, risasi za SMG 47 na maganda yake matatu, maganda ya rifle matano na vichwa vya risasi za rifle  vitatu.
Alisema na nyara za Serikali zilizokamatwa zina thamani ya Sh milioni 120.6.
“Katika msako huu, watuhumiwa 35 walikamatwa na kesi 21 zimefikishwa mahakamani kwa kipindi cha kuanzia Septemba 22, mwaka jana hadi sasa na silaha nyingine zilizokamatwa zilizosalimishwa katika operesheni maalumu iliyofanywa na polisi kwenye wilaya  saba za Mkoa wa Tabora  ni SMG 6, rifle 4, Shotgun 11 na gobole 136,” alisema Seleman.
Naye Waziri Nchemba, alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na kuwataka kuendeleza mshikamano huo ili kukomesha vitendo vya ujangili na ujambazi.
“Maliasili mna dhamana kubwa sana kulinda usalama wa rasilimali zote zilizoko katika hifadhi mbalimbali za serikali vivyo hivyo kwa Jeshi la Polisi, endeleeni na msako huo ili kuhakikisha silaha zote zinazozagaa zinakamatwa mara moja,” alisema Nchemba.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wizara wa Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songorwa, alisema kukamatwa kwa silaha hizo na nyara za Serikali, ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na na taasisi zake za Tawa, Tanapa, NCAA na TFS kwa kushirikiana na polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Alisema wizara hiyo imeanzisha mfumo maalumu wa kupambana na ujangili na uvunaji haramu wa mazao ya misitu kwa kuigawanya  nchi katika Kanda tisa za doria za kiikolojia ambazo ni Selous Kaskazini na Selous Kusini, Serengeti, Burigi-Biharamulo-Rubondo na Katavi-Rukwa-Mahale.
Alitaja kanda nyingine kuwa ni Hifadhi za Taifa Kilimanjaro na Arusha (Momela), Tarangire-Manyara, Ruaha-Rungwa na Moyowosi-Ugalla inayojumuisha wilaya zote zinazozunguka mapori ya akiba ya Moyowosi, Kigosi na Ugalla na zitahusisha za Kibondo, Kakonko, Kaliua, Urambo, Sikonge, Uyui, Tabora, Mlele, Nsimbo, Mbogwe, Ushetu na Bukombe.
Previous
Next Post »