TAARIFA MUHIMU TOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU - Rhevan Media

TAARIFA MUHIMU TOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 25 Januari, 2017 amefungua rasmi awamu ya kwanza ya miundombinu na utoaji wa huduma ya usafiri wa haraka wa mabasi (BRT) katika Jiji la Dar es Salaam uliotekelezwa kwa lengo la kukabiliana na msongamano wa magari ndani ya Jiji na athari zake katika shughuli za uzalishaji mali na ustawi wa jamii.

Mradi huu wa kwanza kutekelezwa Afrika Mashariki na wa tatu Barani Afrika, umehusisha ujenzi wa Kilometa 20.9 za barabara za Kimara – Kivukoni, Fire – Kariakoo na Magomeni – Morocco, vituo vya mabasi 27, madaraja ya waenda kwa miguu 3 na vituo vikuu 3.

Awamu hii ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa miundombinu na utoaji huduma ya usafiri wa haraka wa mabasi imegharimu Shilingi Bilioni 403.5 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 86.5 zimetolewa na Serikali ya Tanzania na Shilingi Bilioni 317 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Utekelezaji wa mradi huu umepangwa kufanywa kwa awamu 6, na awamu ya pili ambayo ipo katika maandalizi ya kumpata mkandarasi baada ya kupata fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), itahusisha ujenzi wa barabara ya kutoka katikati ya Jiji – Mbagala, Magomeni – Chang’ombe na Chang’ombe – Jitegemee. Ujenzi huu utahusisha jumla ya Kilometa 19.3 za barabara na barabara za juu 2 (Flyovers) katika eneo la Chang’ombe na Uhasibu.

Akizungumza kabla ya kufungua rasmi awamu ya kwanza ya mradi huu, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mradi huo katika kipindi chake cha uongozi, na amewapongeza wadau wote waliohusika katika utekelezaji ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Benki ya Dunia iliyotoa mkopo huo.

Mhe. Rais Magufuli ameiomba Benki ya Dunia kuharakisha mchakato wa kutoa fedha za mkopo utakaowezesha kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Ubungo (Ubungo Interchange) ili kuongeza ufanisi wa mradi.

Mhe. Dkt. Magufuli amesema nia ya Serikali yake ni kuifanya Dar es Salaam kuwa Jiji la kisasa kwa kuhakikisha inakomesha tatizo la msongamano wa magari ambapo pamoja na kutekeleza mradi huo pia itajenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kati ya Dar es Salaam na Morogoro na kujenga barabara za haraka (Express Road) kati ya Dar es Salaam na Chalinze hivi karibuni.

“Tunataka Dar es Salaam liwe Jiji la kisasa, ndugu zangu wa Dar es Salaam nataka mniamini hivyo, hivi karibuni tunapitia tenda na tutapata Mkandarasi wa kuanza kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo kuna jumla ya kilometa 200 na treni zitakazopita zitatumia mafuta na umeme”

“Lakini pia mchakato wa kujenga barabara ya haraka (Express Road) kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze yenye njia 6 na hatua zote zimekamilika na kilichobaki ni mazungumzo na wakandarasi kabla ya kuanza kujenga” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika, kuhakikisha mradi huo unaendeshwa kwa faida, miundombinu yake inatunzwa vizuri, wananchi wananufaika kama ilivyokusudiwa na pia ametoa siku 5 kwa Jiji la Dar es Salaam kufanya uamuzi juu ya matumizi ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5.8 zilizotolewa na mbia anayemiliki asilimia 51 ya hisa za kampuni ya UDA-RT.

Pamoja na Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na sherehe hizo zimehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Makhtar Diop ambaye ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza mradi huu muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii na ameahidi kuwa Benki hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara zitakazosaidia kuondoa msongamano wa malori yanayokwenda bandarini kupeleka na kuchukua mizigo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

25 Januari, 2017

Previous
Next Post »