Na MatukiodaimaBlog
MKUU wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah ameanza jitihada za kuhamasisha wananchi wa wilaya hiyo kulima zao la Pareto kama zao la biashara.
Akizungumza na wananchi wa Udekwa na Lulanzi leo, amesema kuwa Kampeni maalum ya kuhamasisha kilimo cha zao La Pareto zimeanza leo kwa kupanda Pareto pia kuona vitalu vya miche ya pareto.
Alisema kimsingi miche hiyo itatolewa bure kwa kila Mwananchi anayehitaji kulima zao hilo.
Alisema pamoja na kupanda mazao mengine ya Chakula na biashara wasiache kupanda japo hekari moja ya zao La Pareto.
Mkuu huyo alisema kuwa zoezi La uhamasishaji upya wa zao La Pareto litafanyika katikati kata mbali mbali za Wilaya ya Kilolo.
Kwani kati ya Wilaya ambazo zilikuwa zikilima zao La Pareto kwa mkoa wa Iringa Wilaya ya Kilolo ni moja ya wilaya ambazo zilikuwa zikilima zao hilo.
Kuhusu soko aliwataka wakulima kuondoa hofu kwani soko kwa sasa ni uhakika
“Nawaagiza mabwana shamba kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kuwapa Elimu juu ya kilimo cha Pareto”
Alisema kuwa zao La pareto limekubali sana Wilaya ya Kilolo kutokana na hali ya hewa ya ubaridi na kuwa zao hilo halihitaji mbolea
Aidha aliwataka wananchi hao kuanzisha vikundi vya kulima zao hilo japo mtu mmoja mmoja anaruhusiwa kulima
“Mimi mwenyewe nitatafuta eneo La kulima Pareto… ila sisemi muache kulima mahindi kwenye heka zako 10 tenga heka moja ya Pareto”
Katika hatua nyingine amewataka wakulima kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kupanda mbegu za muda mfupi zaidi.
Mtaalamu wa Kiwanda cha Pareto Mafinga Godfrey Mbeyela alisema kwa mbegu za Pareto zimeandaliwa na wanategemea wananchi zaidi ya 40 elfu kulima zao hilo.
Alisema kwa wilaya ya Kilolo daraja La chini litanunuliwa kwa Tsh 2000 Kwa wakulima wa Pareto Kilolo
Alisema kuwa soko la Pareto liliyumba kutokana na mwekezaji aliyekuwepo ila sasa soko lipo La uhakika na kuwa pesa zitalipwa kijijini moja kwa moja.
Alisema kuwa kuwa katika Wilaya nyingine kama Ludewa na Njombe wanagombea kulima zao hilo.
Hivyo aliwaomba viongozi wa dini mbali mbali kutumia Nyumba za ibada kuhamasisha wananchi kulima zao hilo.
Kwa upande wao wananchi wa Kilolo wameeleza kufurahishwa na utaratibu huo wa Kiwanda kugawa miche bure na kuwa wapo tayari kuanza tena kulima zao hilo ambalo awali walikuwa wakilima kwa wingi zaidi
|