SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa chama hicho, Abdul Kambaya kutuhuiwna, jana wamerushiana vijembe wakiwa katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na Star Tv.
Wiki iliyopita, aliyeanza kutoa tuhuma alikuwa Mtatiro anayeunga mkono upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye alieleza jinsi ruzuku ya chama Sh milioni 369, ilivyochukuliwa kinyume na taratibu.
Baadaye Kambaya anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alitoa tuhuma za uchotaji mwingine wa mamilioni ya fedha za chama hicho unaodaiwa kufanywa na Mtatiro.
Jana, Kambaya akiwa mgeni Star Tv Mwanza, Mtatiro alishindwa kuhudhuria kwa upande wa Dar es Salaam kutokana na kuumwa ghafla lakini baadaye alizungumza kwa njia ya simu.
Akizungumzia kuhusu walikopata fedha za kuzunguka, Kambaya alisema hawezi kupewa fedha bila kuwa na utaratibu wa kikao.
“Hatuwezi kupewa fedha bila kuwa na utaratibu wa kikao na msajili kuzuia ruzuku alikuwa na sababu za msingi. Wajumbe waliokutana pale Ubungo Plaza tulilalamika kuwa mkutano huo haukuwa ni wa demokrasia.
“Baada ya malalamiko hayo kwa Msajili ndipo alipoamua kusimamisha ruzuku kwa mwezi mmoja.
“Baada ofisi yake kutangaza kumtambua Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa chama aliona mgogoro umekwisha ndipo akatuingizia fedha za ruzuku hizo.
“Ofisi ya Katibu Mkuu iko pale Buguruni, aje pale kufanya kazi. Kwa sasa nafasi ya Maalim anaisimamia Naibu Katibu Mkuu ambaye atatekeleza wajibu wake hadi hapo atakapokuwa tayari,”alisema Kambaya.
Alipoulizwa kuhusiana na utaratibu ruzuku inapoingia, Kambaya alisema: “Zinapangiwa kazi ruzuku wilayani na ndiyo maana Zanzibar wametoa Sh milioni 86 hapo hawakuhusisha mtu zimeenda kufanya uchaguzi. Tuliandika barua kwa msajili tukamweleza, hana sababu tena”.
Wakati anaendelea kutoa maelezo, Kambaya alihama kwenye hoja na kumshambulia Mtatiro na baada ya muda mtangazaji alimtafuta Mtatiro kupitia simu yake kiganjani naye alianza kujibu kama ifuatavyo;
Mtatiro
“Sijawahi kukimbia hata angekuwa Rais Magufuli…Kambaya asijitape sana kwamba naweza kukimbia. Iko haja kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala ya msingi.
“Chama chochote cha siasa kinaongozwa na katiba yake…mgogoro wa CUF ulitengenezwa mwaka 2015.
“Baraza Kuu la uongozi linaweza kuunda kamati maalum si kweli katiba ya CUF haizungumzii Baraza Kuu kuunda kamati yoyote.
“Msajili wa vyama amealikwa na ameshiriki, Kambaya asiseme Baraza Kuu halina uwezo wa kuunda Kamati ya Uongozi.
“Mkutano Mkuu uliandaa agenda, kwanza iliisha ya kukubali kujiuzulu Lipumba. Na ajenda ya kumchagua mwenyekiti ndipo yale magenge ya kukodiwa na watu wenye silaha ndipo tukaahirisha mkutano ule.
“Hao kina Kambaya wamekataliwa na Baraza Kuu na Mkutano Mkuu halafu msajili anawapatia uhalali wao.
“Msajili wa Vyama vya Siasa aliwaandikia makatibu wakuu wa vyama vyote akitaka makatibu wakuu wapeleke akaunti ya vyama .
“Kisheria fedha zinaratibiwa na makatibu wakuu wa vyama hivyo na kama hawana muda wao ndiyo wanakasimu mtu kushughulikia, masuala hayo hayabadilishwi,”alisema Mtatiro.
Mtangazaji wa kipindi hicho alipotaka kusoma maoni ya watazamaji, Kambaya alimkataza asiyasome akisema ni ya vijana wa Chadema.
“Wala usisome hayo maoni najua ya Chadema na hayanipi shida, waliji-organize tangu jana (juzi) na wengine wana akaunti zaidi ya moja kwenye mitandao ya jamii,” alisema.
Akijibu shutuma kwamba amekuwa ni wa kuteuliwa na si kuchaguliwa, Mtatiro alisema:
“Kambaya anasema mimi sijawahi kuchaguliwa bali nateuliwa tu, mimi nimegombea ubunge Segerea uchaguzi uliopita nikachaguliwa kwa kura nyingi na nachangia ruzuku ya chama, yeye atuambie ameleta kura ngapi kuchangia ruzuku?”
Sign up here with your email