Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi.Sihaba Nkinga amekemea vitendo vya Ukeketaji kwa watoto nchini na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria wale watakaobainika.
Akiongea wakati wa Mahafali ya watoto 46 waliokimbia kukeketwa na kujiunga na Kituo cha kulea watoto hao cha ATFGM Kilichopo Masanga Tarime Vijijini Bi.Sihaba alisema kuwa suala la ukeketaji ni kinyume na sheria za nchi na haki za binadamu na ni suala lenye madhara kwa maisha ya watoto.
“Hatukubaliani na suala hili kwani linarudisha maendeleo ya nchi yetu,suala hili pia linachangia kurudisha fikra za vijana wetu na kubatilisha ndoto za vijana wetu, tunao muda wa kujirekebisha na kama tulikuwa tunaendelea basi turudi nyuma”Alisema Bi. Sihaba.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa jamii inayo wajibu wa kulinda na kuendeleza mila zenye kuleta maendeleo na kuacha kulinda na kukumbatia mila zinathoathiri maisha ya binadamu kwani sio suala sahihi kwani mila nyingine zinagharimu maisha ya vijana wetu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga Sister Stella Mgaya akimuonesha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bi. Sihaba Nkinga kifaa cha asili cha muziki kilichotengenezwa na mangariba wastaafu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga Sister Stella Mgaya akiongea wakati wa mahafali ya wasichana 46 waliokimbia ukeketaji na kushukuru juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa wilaya ya Tarime kukabiliana na tatizo hilo, ambapo ameomba wadau kujitokeza kuwaendeleza watoto wanaohitimu kituoni hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bi.Lydia Bupilipili akiongea wakati wa mahafali ya wasichana 46 waliokimbia ukeketaji na kuwasisitiza wazazi na walezi kubadilika na kuachana na imani potofu ya ukeketaji ili kuwawezesha wasichana kutimiza malengo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Glorious Luoga akiongea wakati wa mahafali ya watoto waliokimbia kukeketwa na kujiunga katika kituo Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga ambapo aliwataka wazazi wanaowatenga na kulazimisha kukeketa watoto wa kike waliohitumu mafunzo kuacha tabia hiyo kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bi. Sihaba Nkinga akiongea wakati wa mahafali ya watoto waliokimbia kukeketwa na kujiunga katika kituo Watoto waliokimbia Kukeketwa cha ATFGM-Massanga, ambapo alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wazazi na jamii inayoendelea na kitendo kiovu cha ukeketaji kwa watoto wa kike.
Sign up here with your email