Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema hana hofu ya kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake, huku akisema msimamo wake uko palepale na kwamba anamtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif ni Katibu Mkuu.
Kauli ya Jaji Mutungi imekuja baada ya taarifa na kauli za matusi na kejeli zilizomuhusisha yeye na ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh300 milioni za ruzuku kwenda kwenye akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF ilidai siyo ya chama hicho.
Taarifa za msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa kwa njia ambayo inaonekana kutia shaka zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alilinganisha suala hilo na uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Kupitia taarifa yake jana, Jaji Mutungi alisema kuna mbinu zinazopangwa na wanaojiita Kamati ya Uongozi ya CUF ambayo ofisi yake haiitambui, huku akisisitiza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu.
Jaji Mutungi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifunguliwa kesi Mahakama Kuu na bodi ya wadhamini wa CUF ikiiomba itoe amri ya kubatilisha barua ya mlezi huyo wa vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, alisema kauli zinazotolewa mitandaoni zina lengo la kuchafua ofisi yake.
“Tayari mbinu hizo zimeanza kutekelezwa na viongozi wa kamati hiyo kwa kusambaza habari za kudhalilisha katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kama Facebook na mingineyo,” alisema.
Msajili huyo alisema moja ya mkakati huo ni taarifa iliyosambazwa juzi na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF,, Mbarala Maharagande ya kejeli, matusi, tuhuma na dhihaka kwake.
Jaji Mutungi alisema hivi karibuni, Maharagande alizungumza na waandishi wa habari huku akidai kuwa ofisi ya msajili inasababisha mpasuko ndani ya chama hicho na ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Profesa Lipumba.
Licha ya tuhuma hizo, Jaji Mutungi alisema kwamba haogopi kuchafuliwa akizingatia ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake akiwatumia wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema kamwe hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli zinazotolewa dhidi yake pamoja ofisi anayoiongoza.
“Nimezipata hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa kunichafua, japo naendelea kuzifanyia kazi lakini waache wanichafue, wala siogopi lolote,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema mjadala wa ruzuku ya CUF aliyotoa kwa chama hicho ameshaufunga na anashangazwa na maneno yanayozidi kusambazwa na watu wanaojiita viongozi wa CUF.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Maharagande aliendelea kusisitiza kuwa kauli iliyotolewa wakati alipofanya mkutano na vyombo vya habari ipo hivyo na kwamba waliitisha mkutano kumjibu msajili ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari siku moja kabla kuhusu masuala ya CUF.
Sign up here with your email