MPINZANI WA NAPE 2015 AFUNGWA JELA - Rhevan Media

MPINZANI WA NAPE 2015 AFUNGWA JELA


Mtzd Design Friday templateSiah.indd

MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi, imemuhukumu kwenda jela miezi nane, Suleiman Mathew ambaye alikuwa mpinzani wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 katika Jimbo la Mtama.
Mathew ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Lindi na kiongozi mwenzake wa kata wamehukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mkusanyiko bila ya kibali.
Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama ya Mkoa wa Lindi, mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mhina.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza mashahidi sita wa upande wa mashtaka na kujiridhisha kuwa ushahidi wao umethibitika bila kuacha shaka.
Waliotiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo ni Mwenyekiti Chadema mkoani Lindi, Selemani Methew pamoja na Katibu wa Tawi la Kata ya Nyangamala, Ismail Kupilila.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mhina alisema, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Juma Maige uliwafikisha mahakamani hapo mashahidi sita.
Alisema kutokana na ushahidi ulitolewa na mashahidi hao, mahakama imeona upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao bila kuacha shaka yoyote na kuwatia hatiani.
Baada ya kuwatia hatiani mahakama iliwapa nafasi washtakiwa ili waweze kujitetea ambapo waliomba  wapunguziwe adhabu.
Akiwasilisha hoja za upande wa utetezi Wakili wa washtakiwa hao,  Deusdet Kamalamo aliiomba mahakama isiwape adhabu kali kwa madai kwamba wanafamilia inawategemea, hivyo iwapo watapewa adhabu kubwa kutaifanya ikose huduma zao.
Baada ya utetezi huo, Wakili wa Serikali Juma Maige aliiomba mahakama hiyo iwape washtakiwa hao adhabu kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza ili iwe fundisho kwao na wengine.
Hakimu Mhina akitoa adhabu katika kesi hiyo namba 36/2016, chini ya kifungu cha 74 (1) na 75 cha kanuni ya adhabu sura ya 16, alisema mahakama inawapa adhabu, kila mshtakiwa  atatumikia kifungo cha miezi minane gerezani na kusema nafasi ipo wazi ya kukata rufaa iwapo wataona hawakuridhishwa na hukumu hiyo.
Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Mathew alisikika akiguna na baadae aliketi sakafuni, huku katibu wake wa tawi, Ismail  ambaye alionekana kuchoka kutokana na hukumu hiyo akiwa amelowa kwa jasho.
Mahakama hiyo pia iliwaachia huru washtakiwa wanne ambao ni wanachama waliokuwa wameshtakiwa pamoja na viongozi hao, baada ya ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa mashtaka kutokuwa na mashiko ya kuishawishi mahakama kuwatia hatiani.
Washtakiwa hao ni Bashiru Rashid, Hassani Mchihima, Abdallah Masikini na Mohamedi Makolela ambao wote ni wakazi na wakulima wa Kata ya Nyangamala.
Awali washtakiwa hao walidaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3,  mwaka jana, maeneo ya Kata ya Nyangamala, mkoa Lindi, washtakiwa walifanya mkusanyiko usio halali.
Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Wakili wa upande wa utetezi,  Deusde Kamalamo alisema wanajiandaa kukata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo.
“Tutakata rufaa kupinga uamuzi huu, leo naandaa barua ya kuomba nakala ya hukumu ili tuanze kuandaa rufaa ya wateja wangu,” alisema Wakili Kamalamo.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Methew alikuwa akipambana na Nape ndani ya CCM lakini alishindwa kufurukuta katika kura za maoni na baadae alijiengua na kujiunga na Chadema na kuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho.
Katika hatua nyingine jana Diwani wa Kata ya Kyangasaga, wilayani Rorya, Christopher Kichinda maarufu ‘Protocol’ amehukumiwa kwenda jela miaka mitano.
Akizungumzia hukumu hiyo Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche, alisema diwani huyo alikuwa anakabiliwa na kesi ya Katiba iliyokuwa inamkabili kuwa alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya lakini alijitoa ambapo mahakama ilimtia hatiani kwa makosa yaliyokuwa yanamkabili.
“Ni kilio kingine kwa demokrasia ya nchi yetu na ufanisi kwa siasa za CCM,” alisema Heche.
Mbali na viongozi hao wiki iliyopita Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ilimuhukumu Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (30), kifungo cha miezi sita kwa kufanya vurugu na kusababisha taharuki kwenye mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi, Dotto Ngimbwa awali alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa namba moja (Peter) na mwenzake Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi, mwaka jana Kibaoni kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
MBOWE ALAANI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akizungumzia hatua ya Methew kuhukumiwa kwenda jela, alisema huo ni
mkakati ulioandaliwa Serikali ya CCM kudhohofi sha upinzani na kuwatisha wasifanye siasa.
Hata hivyo, Mbowe aliwagiza viongozi wa chama hicho nchi zima kuandaa orodha ya kesi walizonazo ili kuziwasilisha jumuiya
za kimataifa kuonyesha jinsi upinzani unavyokandamizwa na kupokonywa haki yao ya kufanya siasa.
Alisema Methew amehukumiwa wakati tayari Mbunge wa Kilombero, Peter Lijuakali akiwa ameshahukumiwa kwenda jela miezi sita.
Previous
Next Post »