MIKATABA 9 TANZANIA NA UTURUKI YASAINIWA - Rhevan Media

MIKATABA 9 TANZANIA NA UTURUKI YASAINIWA


Nchi za Tanzania na Uturuki leo zimetiliana saini mikataba tisa ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo leo baada ya kuwasili kwa Rais wa Uturuki kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini.

Bendera za Uturuki na Tanzania

Akizungumza baada ya kutiliana saini mikataba hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema, ujio wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan umejumuisha wafanyabiashara 150 na kwamba, mikataba iliyosainiwa itasaidia kukuza uchumi pamoja na mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Rais Magufuli ameitaja baadhi ya mikataba iliyosainiwa kuwa ni ya sekta za afya, elimu, ulinzi, na viwanda ambapo amesema, amemuomba Rais Erdogan kuikopesha Tanzania kiasi cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge yenye urefu wa zaidi ya kilometa 400.
Rais Magufuli pia amesema Rais huyo wa Uturuki amekubali kuongeza nafasi za wanafunzi wanaokwenda kusoma nchini Uturuki kutoka idadi ya wanafunzi 48 iliyopo hivi sasa, na katika masuala ya ulinzi, amesema Uturuki imekubali kutoa mafunzo ya ulinzi kwa watanzania nchini Uturuki.
Hadi sasa kampuni 30 za Uturuki zimefanya uwekezaji nchini Tanzania wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959 na hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 mwaka 2009 na kuwa  Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352.
Previous
Next Post »