Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Doto Mashaka Biteko (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja wa Mgodi wa Buzwagi, Assa Mwaipopo (hayupo pichani) akielezea shughuli za uzalishaji wa Dhahabu katika Mgodi huo. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na wengine ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Watumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Wafanyakazi wa Mgodi wa Buzwagi.
Kaimu Kamishna wa Nishati na Madini, Ally Samaje (anayetoa maelezo) akielezea Mpango wa Serekali wakati wa kufunga Mgodi wa Buzwagi. Wengine katika picha ni Wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na Viongozi Waandamizi kutoka Mgodi wa Buzwagi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Ntalikwa (katikati) akiwa anafanya majadiliano na Kaimu Kamishna wa Madini, Ally Samaje na Mbuge wa Kahama Jumanne Kishimba Mara baada ya kutembelea mgodi wa Buzwagi.
Wataalamu kutoka Idara ya Madini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutoka katika eneo la uzalishaji wa Dhahabu.
Muonekano wa Mgodi wa Buzwagi katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,
Kotena iliyofanyiwa maandalizi tayari kupokea makinikia ya Shaba ambayo yanachimbwa kwa asilimia kubwa katika Mgodi wa Buzwagi.
Kotena ambayo tayari imejazwa na makinikia ya Shaba tayari kwa ajili ya kufunga ili kusafirishwa nje.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Ntalikwa (wa pili kushoto) akimsikiliza Kaimu Kamishna wa Madini Mhandisi Ally Samaje, kabla ya kusikiliza mada kutoka kwa Meneja wa Buzwagi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Doto Mashaka Biteko (wa pili kulia) akiwa na wanakamati wezake wakiongozana na Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Mgodi wa Buzwagi mara tu baada ya kuwasili katika Mgodi huo.
……………………
Na Rhoda James – Kahama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa ameuongoza ujumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Wizara ya Nishati na Madini ili kukagua na kuhoji utendaji na ushiriki wa mgodi wa Buzwagi katika masuala ya kijamii mkoani Shinyanga hivi karibuni.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeutaka Uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kuwashirikisha wananchi pamoja na wafanyakazi wa Mgodi huo Mpango wa kuufunga Mgodi huo (Mining Closure plan) unaotarajia kufunga shughuli zake za uzalishaji wa Dhahabu ifikapo Desemba 2017, huku shughuli za uchejuaji zitaendelea kwa miaka miwili.
Haja hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Doto Mashaka Biteko mara baada ya kuwasili na kukutana na uongozi wa mgodi huo wakati wa ziara hiyo ya ukaguzi wa mgodi huo.
Biteko alisema kuwa Wananchi na wafanyakazi lazima wawe sehemu ya ufungaji wa Mgodi huo kwa kuwa jambo hilo ni kubwa kwani litatikisa Uchumi wa wananchi wa Kahama na pia Halmashauri ya Kahama itakosa Ushuru wa Huduma ambazo Mgodi huo umekuwa ukilipa kila mwaka.
“Mgodi huo unalipa Ushuru wa Huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama na wafanyakazi katika mgodi huo wana ajira kwa hiyo mipango ya kufunga mgodi huo iwe sehemu ya wananchi kwa asilimia mia” alisisitiza Biteko.
Aidha Biteko alitaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa Uongozi wa Mgodi huo ni sababu zipi zinazopelekea mgodi huo kufungwa. Vilevile, alitaka Uongozi kuijulisha kamati hiyo jambo ambalo mgodi huo unawaachia wanannchi wa Kahama mara baada ya shughuli za uzalishaji kufungwa.
Akijibu hoja hizo Meneja wa Mgodi wa Buzwagi, Assa Mwaipopo alisema kuwa Serikali na wananchi wamekuwa wakishirikishwa kikamilifukakita shughuli mbalimbali za mgodi huo ikiwemo kuhusu nini kifanyike baada ya kufunga mgodi. Alieleza kuwa, Mgodi na Serikali wanansubiri maoni ya wananchi kuhsu shughuli sahihi za kufanya katika eneo hilo la mgodi mara tu utakapomaliza shughuli zake.
Mwaipopo alifafanua kuwa ingawa mgodi umekuwa ukipata faida kutokana na shughuliza uchimbaji dhahabu bado mgodi hsujarudisha gharama za awali ambazo zilitumika wakati wa uwekezaji huo.
Akijibu swali la mjumbe mwingine wa kamati ya Bunge aliyehoji juu ya malalamiko ya wafanyakazi wa mgodi huo kutokujua mwajiri wao kwa kuwa mikataba yao inaonesha ni kati yao na Pangea Mining Gold, vitabulisho vyao vinatoka African Barrick Gold Mine na malipo yao yanaonesha yanalipwa na Acacia Mining Gold. Mwaipopo alisema kuwa mmiliki wa Mgodi huo ni Pangea na ndiye anayewajibika na huyo ndiye mwaajiri wao.
Aidha Kamati ya Kudumu ya Wizara ya Nishati na Madini iliitaka Wizara kutoa ufafanuzi wake ni kwa nini Mgodi wa Buzwagi unaendelea kubadili majina kama vile Pangea, African Gold Mine na Acacia Gold Mine.
Akitoa ufafanui wa suala hilo, Kaimu Kamishna wa Madini, Ally Samaje alisema kuwa mgodi unapobadili jina au anwani basi haina madhara lakini pale unapobadili umiliki wake, lazima mchakato huo wote ushirikishe serikali na upate ridhaa ya serikali kwa kuwa hapo kuna ulipaji wa Kodi na Mapato mbalimbali kwa serikali.
Ziara hii ni wiki moja inayowawezesha wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Wizara ya Nishati na Madini kukagua na kuhakikisha wizara wanazozisimamia zinatekeleza majukumu yao kama inavyowapasa.
Sign up here with your email