Sheria inaruhusu kutumia ardhi ya mtu kukopea. Kwa maana mtu ataomba hati yako au nyaraka yako yoyote ile ya umiliki halafu ataitumia kukopea. Inaitwa Rehani ya mtu wa tatu( third party mortgage). Kifungu cha 113 ( 2 ) cha Sheria ya Ardhi Na, 4 ya 1999 kimeeleza kitu hiki. Hata hivyo yapo mambo tunayotakiwa kujua katika mchakato huu wote.
Ili mambo yaende vizuri kutatakiwa kuwapo mikataba ya aina tatu kama tutakavyoona hapa chini.
1.MKATABA WA MKOPO.
Mkataba wa mkopo ( Loan agreement) ni mkataba kati ya mwomba mkopo na na taasisi ya fedha inayotakiwa kutoa mkopo.
Mkataba huu utakuwa na masharti ya mkopo kuhusu urejeshaji, muda wa kurejesha, viwango vya riba, adhabu za kupitisha muda wa rejesho, muda ambao mkopo utadumu, nini kitafanyika iwapo mkopaji atashindwa kurejesha, haki na wajibu wa mkopaji pamoja na mkopwaji.
Ifahamike kuwa masharti ya mkopo hayafanani. Yanatofautiana kutoka taasisi hadi taasisi na pia yanatofautishwa na kiwango cha mkopo pamoja na mazingira yote yanayouzunguka huo mchakato. Huu ni mkataba wa kwanza.
2. MKATABA WA REHANI.
Huu ni mkataba wa pili. Mkataba wa rehani ( mortgage deed ) utakuwa ni kati ya taasisi ya fedha na mtu anayeweka rehani. Kwahiyo kama wewe unamdhamini mtu kwa kumpa nyumba au shamba lako ili akakopee basi unatakiwa kusaini mkataba huu.
Yule ambaye jina lake linaonekana kwenye nyaraka ya umiliki ndiye anayetakiwa kusaini mkataba huu.
3. MKATABA KATI YA ANAYEDHAMINI NA ANAYEDHAMINIWA.
Aidha usimkabidhi mtu hati yako akakopee bila kuwa na makubaliano ya kisheria na huyo mtu. Ni hatari sana kufanya hivi na unaweza kupoteza na wengi wamekwishapoteza.
Wengi wanachojali ni mtu achukue hela benki na wewe akupe asilimia zako mlizokubaliana basi muishie hapo. Ukifanya hivi utakuwa umekosea sana.
Wengine huaminiana tu kwa urafiki au undugu na kufanya mchakato huu bila makubaliano maalum. Hii si sawa na ina madhara makubwa.
Hakikisha unamsainisha mkataba huu na hakikisha mkataba unakuwa na vipengele muhimu na vya kisheria vya kukulinda wewe na mali yako.
Moja ya kipengele muhimu ni kueleza wazi ikiwa atashindwa kulipa deni huko alikokopa ni kitu gani kitakulinda ili mali yako isiuzwe au hata ikiuzwa wewe utapata nini kutoka kwake kufidia hiyo hasara.
Sign up here with your email