LEMA NA MKEWE WAKANA MASHITAKA DHIDI YA .... MAWAKILI WAKE WAOMBA KESI IPELEKWE MAHAKAMA YA KATIBA - Rhevan Media

LEMA NA MKEWE WAKANA MASHITAKA DHIDI YA .... MAWAKILI WAKE WAOMBA KESI IPELEKWE MAHAKAMA YA KATIBA

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) jana alikana tuhuma za makosa ya jinai kwa pamoja na mkewe, Neema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Nestory Barro, Lema na Neema walikana mashtaka ya kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi wenye matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Awali akiwasomea maelezo ya kesi hiyo Wakili wa Serikali Alice Mtenga alidai kuwa Lema na Neema, Agosti 20 mwaka jana, ndani ya Jiji la Arusha, walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani kwa mkuu huyo wenye lugha ya matusi, huku wakijua ni kosa kisheria.

Ilidaiwa kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka simu namba 0764-150747 kwenda namba 0766-757575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga.”

Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo na tarehe ya kukamatwa kwao.

Hakimu Barro aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, ambapo upande wa Jamhuri utaanza kuwasilisha ushahidi wake Gambo akiwa wa kwanza.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wakili wa Lema, John Mallya aliiambia mahakama wanatoa notisi ya kuwasilisha pingamizi la mdomo kwa kuwa hati ya mashtaka ina mapungufu, na baadaye wataomba mahakama iitupilie mbali hati hiyo.

Hata hivyo, Hakimu huyo alisema hoja za awali za pingamizi hilo zitasikilizwa Februari 3 pia.

Mbali na Mkuu wa Mkoa, Jamhuri inakusudia kuita mashahidi wengine wanne, ilielezwa.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mtenga upande wake pia utakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa
mahakamani hapo.

Alisema mashahidi watano watakaotoa ushahidi wao ni Gambo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, (ASP) Damasi Massawe, mhusika kutoka kampuni ya simu ya Vodacom pamoja na mtaalamu wa picha.

Pia alivitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya taarifa za mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, simu ya mshtakiwa mke wa Lema na taarifa ya uchunguzi kutoka kitengo kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).

Wakati huo huo, wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, John Mallya amemuomba Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Bernard Nganga kutoanza kusikiliza kesi ya kuhamasisha maandamano Septemba Mosi (Ukuta) inayomkabili Lema peke yake.

Akitoa ombi hilo jana, Mallya alidai kuwa kesi hiyo ya kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao wa kijamii kisha kuusambaza Agosti Mosi hadi Agosti 26 mwaka jana, haifai kusikilizwa katika mahakama hiyo sababu kuna hoja za Kikatiba.

Alisema shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi wake ambaye ni RCO, George Katabazi hapaswi kutoa ushahidi mahakamani hapo, sababu kesi hiyo ina hoja za kikatiba.

“Mheshimiwa kesi hii ukiiangalia ipo kikatiba zaidi na kwasababu ipo kikatiba basi sisi tunaenda Mahakama Kuu ikasikilizwe na majaji watatu ili tupewe tafsiri ya vifungu vya sheria," alisema Mallya.

Alisema kwa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 inampa haki kiongozi au mwanasiasa kufanya shughuli za kisiasa.

"Kuwakataza au kuingilia kati tunataka kujua huko Mahakama Kuu ya Katiba, nani ana mamlaka ya kuzuia maandamano."

Naye wakili wa Serikali Mtenga alimuomba hakimu kutupa pingamizi la Mallya alilolitoa mahakamani hapo, badala yake kesi hiyo iendelee kusikilizwa kwani upande wa Jamhuri tayari ulishamuandaa
shahidi wake.

Hakimu Nganga alisema amesikia hoja za mawakili hao wa pande zote mbili na yeye anaendelea na kesi hiyo baada ya aliyekuwa
 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augutino Rwezile kupanda cheo na kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha biashara.

Alisema atatoa uamuzi wa kesi hiyo, kusikilizwa au kwenda kwa majaji watatu Februari 8.
Previous
Next Post »