Picha zilizopigwa nchini Iraq zinaashiria kwamba huenda wapiganaji wa kundi linalojiita Islamic State wanatumia ndege zisizo na rubani kutekeleza mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Iraq.
Ndege zinazotumiwa ni ndege za kawaida ambazo zinaongezewa bomba fupi la plastiki kwenye kamera na kutumiwa kubeba vilipuzi.
Picha hizo zilipigwa na mwanajeshi wa zamani wa Marekani Mitch Utterback, ambaye alirejea Iraq kama mwanahabari.
Wiki iliyopita, kamanda mmoja wa wanajeshi wa Marekani alisema IS wanatumia ndege kama hizo kujaribu kuendelea kudhibiti mji huo.
"Si kwamba ni ndege kubwa ambayo inaangusha mabomu, ni ndege ndogo tu ambayo inaangusha silaha ambazo si nzito kwa ufasaha sana," alisema kanali Brett Sylvia.
Islamic State awali wamekuwa wakitumia ndege zisizo na marubani kupiga picha kutoka angani na pia kuchukua video za kutumiwa kwenye propaganda.
Aidha, wamekuwa wakitumia ndege kama hizo kufanya upelelezi kando na kuzitumia kama vilipuzi.
Oktoba, wapiganaji wawili wa Kikurdi waliuawa kaskazini mwa Iraq baada ya ndege isiyo na rubani iliyokuwa imefanyiwa ukarabati kulipuka.
Ndege nyingi za kawaida zisizohitaji marubani, ambazo huuzwa madukani, zinaweza kusafiri kwa maili kadha.
Huwa zinauzwa chini ya £1,000. jambo linaloifanya kuwa rahisi kwa makundi ya wapiganaji kuzitumia.
Sign up here with your email