KAVAZI LA MWALIMU NYERERE KUADHIMISHA MIAKA 50 YA AZIMIO LA ARUSHA - Rhevan Media

KAVAZI LA MWALIMU NYERERE KUADHIMISHA MIAKA 50 YA AZIMIO LA ARUSHA



KAVAZI LA MWALIMU NYERERE linayo furaha kuwakumbusha Watanzania, Waafrika na wapenda haki na usawa duniani kwamba ifikapo tarehe 5 Februari 2017, Azimio la Arusha litakuwa limefikisha miaka hamsini, au nusu karne, tangu kuzaliwa kwake. Kama njia ya kuadhimisha miaka hamsini ya Azimio, KAVAZI limepanga kuandaa mazungumzo ya siku mbili, kuanzi tarehe 22 hadi 23 Februari mwaka huu. Mazungumzo hayo yatafanyika katika ukumbi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 9 alasiri. Mada kuu itakuwa: Simulizi za Azimio la Arusha.

Azimio la Arusha lilikuwa waraka mojawapo wa kimapinduzi ulioandaliwa na kutekelezwa barani Afrika. Aidha, katika mazingira ya mapambano ya ukombozi ya wakati huo, Azimio liliwafarijisha na kuwatumainisha Waafrika kote duniani. Kama uhuru wa Ghana ulirejesha heshima ya Mwafrika, kama alivyosema C.L.R. James, mwanamajumui maarufu, basi Azimio lilikuwa ni matumaini ya mnyonge kujikomboa kutokana na makucha ya unyonyaji wa ndani na wa kibeberu. Kauli mbiu ifuatayo ya Azimio ilipokelewa kwa shangwe, ikawa wimbo wa kitabaka wa wavujasho:

Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena.

Kwa kulitumia Azimio kama dira na itikadi ya ukombozi na maendeleo, viongozi wa kisiasa wa kizazi cha kwanza, waliahidi na kudhamiria kwa dhati kujenga jamii na nchi ya kijamaa inayoheshimu na kulinda misingi ya usawa wa binadamu wote; isiyo na ubaguzi wa aina yoyote na isiyo na unyonyaji. Yaani nchi ya kijamaa, inayojitegemea, isiyo na matabaka ya wanyonyaji na wanyonywaji, au kwa maneno mengine, wavunajasho na wavujajasho

Ni matarajio yetu kwamba mazungumzo hayo ya siku mbili ni fursa adhimu kwa washiriki kukumbushana kuhusu historia ya mapambano ya ukombozi na ujenzi wa taifa na bara lao. Aidha, washiriki watasimuliana, watajadiliana, watatafakari, watadadisi na kulichambua Azimio pamoja na kuainisha mafunzo yanayotokana na falsafa, itikadi pamoja na utekelezaji wake. Wote mnakaribishwa.

Issa Shivji (Profesa)
Mkurungezi, Kavazi la Mwalimu Nyerere, COSTECH


Previous
Next Post »